MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mikuu sita ya Taasisi.
Ndomba alisema hayo wakati wa kikao cha Watumishi wa Mamlaka kilichofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa umma
Alisema kuwa e-GA inaongozwa na misingi mikuu sita ambayo inaelekeza kuhusu tabia na mwenendo wa watumishi wake kwa ngazi zote na kufafanua utamaduni wa mahali pa kazi ili kuhakikisha watumishi wote na wateja wa Mamlaka wanaouelewa wa pamoja wa jinsi wanavyotakiwa kuhudumiwa na nini kinachotarajiwa kutoka kwao.
"Nawakumbusha watumishi wote wa Mamlaka kuzingatia misingi hiyo ambayo ni uadilifu, ubunifu, kutathmini wateja, ushirikiano, kufanya kazi kwa pamoja na weledi katika utendaji kazi wao wa kila siku,"alisema Ndomba.
Alisema kuwa Mamlaka imekuwa taasisi ya mfano inayofanya shughuli zake za kila siku kwa kasi na ari inayokubalika, kutokana na uadilifu mkubwa wa Menejimenti na watumishi waliodhamiria kuweka juhudi kubwa katika kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji huduma bora kwa umma.
“Nawakumbusha watumishi wote kuimarisha uadilifu na kila mtumishi na kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kwa weledi kwa kuzingatia misingi hiyo huku Mamlaka ikiendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa watumishi wanafanya kazi katika mazingira bora na salama,”alisema Ndomba.
Aidha alisema kuwa katika kikao hicho mada mbalimbali zilizolenga kujenga uelewa na ufahamu kwa watumishi ziliwasilishwa ikiwemo Afya mahali pa kazi, Rushwa mahala pa kazi, Maadili ya utendaji, Haki na Wajibu, HIV/AIDS na magonjwa sugu yasiyoyakuambukiza, mawasiliano mazuri kwa utendaji bora wa kazi, namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo na maisha kazini.
Kikao hicho kilihitimishwa na Bonanza la Michezo lilifanyika katika viwanja vya Gymkana ambapo michezo mbalimbali ikiwemo kukimbiza kuku, kuvuta kamba, kukimbia kwa kutumia magunia, kukimbia na yai kwenye kijiko na mbio fupi.
No comments:
Post a Comment