CHAMA Cha Madereva Wanawake Tanzania (CWMT) kinatarajia kuanzisha kampuni ya usafirishaji ili kujiongezea kipato na kutoa ajira kwa wanachama wake.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa chama hicho Naetwe Ihema alisema kuwa lengo ni kumkwamua mwanamke ili ajitegemee na asiwe tegemezi.
Ihema alisema kuwa madereva wanawake kwa sasa ni wengi ambao wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Taasisi za serikali na binafsi lakini walikuwa hawana Umoja wao.
"Tumeanzisha chama hichi ambacho mwanzo ilikuwa ni kikundi tukaona tujiongeza na kuwa chama ambacho kimesajiliwa na moja ya malengo yetu ni kuwa na kampuni ya usafirishaji kwa mabasi ya kwenda mikoani na daladala ambapo wanachama wetu watakuwa ndiyo madereva,"alisema Ihema.
Alisema kuwa wanatarajia kuongea na watu wenye kampuni za mabasi kwa kuanzia mabasi madogo (daladala) ili waingie makubaliano kama ni kuwakopesha au njia yoyote ili waweze kupata mabasi ili waanze kufanya hiyo kazi.
"Tutaanzisha hiyo kampuni ya usafirishaji kwani ajira kwa madereva wanawake ni changamoto ambapo waajiri wanakuwa hawawaamini wanawake lakini ni madereva wazuri na uwezo wao ni mkubwa,"alisema Ihema.
Aidha alisema kuwa madereva wanawake hawasababishi ajali kutokana na kuwa makini na hofu ya kuogopa kupoteza uhai wa watu ndiyo sababu udereva wao ni wa kujihami na siyo kujiamini.
"Mafanikio tuliyoyapata kwa mtu mmoja mmoja ni kuweza kuhudumia familia ambapo kwa wale walioolewa wanauwezo wa kushirikiana na waume zao katika kuendesha maisha na ambao hawajaolewa wanasomesha, wamejenga na wanafanya maendeleo makubwa,"alisema Ihema.
Aliongeza kuwa sifa ya mwanachama awe anaendesha chombo chochote cha moto ambapo baadhi ya wanachama wao ni marubani wa ndege, manahodha wa meli, madereva wa mitambo ya ujenzi, magari ya mizigo, mabasi makubwa, madereva wa treni, madereva wa uba, madereva wa mwendokasi na magari ya watu binafsi. Chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 na kina wanachama 120.
No comments:
Post a Comment