Wednesday, March 1, 2023

WALIMU KUZAWADIWA VIWANJA



KATIKA kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne hawapati sifuri Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema itatoa viwanja kwa walimu shule zao zitakazofanya vizuri.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa elimu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha kilichofanyika Kibaha alisema kuwa kuna changamoto katika ufuaulu na masomo ya Sayansi.

John alisema kuwa lengo ni kuondoa asilimia 50 ya wanafunzi ambao wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kutofanya vizuri kwenye mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne.

"Tutatoa viwanja kwa walimu ambao watafanya vizuri kwa kuongeza ufaulu ambapo tungetamani kusiwe na daraja sifuri na daraja la nne kwani madaraja haya yanawafanya wasiweze kuendelea na masomo tunataka angalau kuanzia daraja la tatu na kupanda juu,"alisema John.

Alisema kuwa mbali ya kutoa viwanja pia kutakuwa na motisha mbalimbali zitatolewa ikiwemo fedha taslimu kwa walimu watakaofanya vyema na mkazo utawekwa kwenye masomo ya Sayansi ambayo matokeo yake siyo mazuri.

"Pia tunataka Mwalimu anapaswa kuhakikisha mwanafunzi katika somo lake apate alama C na kama atashindwa kufikia hapo itabidi aulizwe changamoto ni nini,"alisema John.

Aliwataka wazazi na wadau wa elimu kushirikiana na shule ili kufanikisha kuondoa sifuri kwenye shule za sekondari zilizokwenye Halmashauri ya Mji Kibaha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Musa Ndomba alisema kuwa uongozi wa shule ukabili changamoto na siyo kulalamika hata kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wao.

Ndomba alisema kuwa watahakikisha mipango na mikakati iliyowekwa wanaitekeleza ili kuondoa matokeo mabaya kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari ili kupata wasomi watakaoshiriki kwenye uchumi ikizingatiwa mkoa wa Pwani ni wa viwanda.

Awali ofisa Elimu Halmashauri ya Mji Kibaha Rosemary Msasi alisema kuwa ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa kipindi cha miaka mitano 2018 hadi 2022 umeongezeka.

Msasi alisema kuwa ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 7.89 kwa kutoka asilimia 84.4 hadi asilimia 92.2 na ule wa kidato cha sita kutoka asilimia 99.4 hadi asilimia 100.9.

Baadhi ya walimu wakuu ambao shule zao zilifanya vizuri walisema kuwa kikubwa ni ushirikiano uliopo baina ya walimu wazazi na wanafunzi na Halmashauri.

Kikao hicho cha wadau baadhi ya walioshiriki ni pamoja na kamati ya usalama Wilaya, maofisa elimu wa Kata, watendaji wa kata, wakuu wa shule za msingi na sekondari.

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment