Sunday, March 5, 2023

WATATU WAFA AJALINI WAMO ASKARI POLISI WAWILI

WATU watatu wakiwemo askari wawili wa Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa watu hao walifariki papo hapo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Machi 5 mwaka huu majira ya saa 11:45 alfajiri huko maeneo ya Mavi ya Ng'ombe Kijiji cha Mboga Kata ya Msoga Tarafa ya Chalinze katika Barabara ya Chalinze/Segera.

"Gari lenye namba za usajili T 323 BAL aina ya Toyota Cresta likiendeshwa na mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28) askari wa kituo cha Polisi Chalinze akitokea Chalinze kuelekea Lugoba liliacha njia kutoka upande wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia na kugonga kalavati kisha kupinduka na kusababisha vifo vya watu watatu na mmoja kujeruhiwa,"alisema Lutumo.

Aliwataja askari waliokufa kuwa ni Mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28) aliyekuwa dereva wa gari hilo, Konstebo  Emmiliana Charles (26) wote askari wa kituo cha Polisi Chalinze na Karimu Simba (27) ambaye ni karani wa Mahakama ya Wilaya Lugoba.

"Majeruhi huyo ambaye naye  ni askari wa Kituo cha Polisi Chalinze Konstebo Mwanaidi Shabani (25) ameumia maeneo mbalimbali ya mwili wake na amepelekwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi,"alisema Lutumo.

Aidha alisema kuwa uchunguzi wa awali umeweza kubaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na dereva kushindwa kulimudu gari na kupinduka.

"Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Lugoba kwa ajili ya kusubiri taratibu za mazishi,"alisema Lutumo.

No comments:

Post a Comment