Wednesday, March 1, 2023

WATENDAJI KATA WAKABIDHIWA PIKIPIKI

HALMASHAURI ya wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani imewapatia Pikipiki watendaji wa Kata tano ili kuondoa changamoto ya kushindwa kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.

Akikabidhi Pikipiki hizo kwa watendaji hao wa Kata katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mbunge wa Kibaha Vijijini Michael Mwakamo amewataka watendaji kuzitumia pikipiki hizo kama ilivyokusudiwa na serikali na siyo kwenda kuzifanya boda boda.

Mwakamo amesema kuwa pikipiki hizo ni kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuondoa changamoto ya usafiri kwa watendaji kata ili kuwarahisishia majukumu yao. 

"Niwasihi watendaji waliopewa pikipiki leo mkazitumie kama ilivyokusudiwa na tusizikute zimebeba abiria mtaani maana siyo nia ya kukabidhiwa bali ni kutekeleza majukumu ya kazi zenu,"amesema Mwakamo.

Amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha wanawasaidia kwenye matengenezo na kuwawekea mafuta pikipiki hizo kwani ni vyombo vya kazi na wasivitumie kama vyombo binafsi. 

Awali Mwakamo aliishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi ya kutoa vitendea Kazi kwa watendaji wa ngazi zote Ili kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Umama.Kata zilizopokea pikipiki ni Soga, Magindu, Kwala, Gwata na Dutumi ambazo ni kata zilizopo pembezoni mwa Halmashauri.

No comments:

Post a Comment