JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili ambao wamemaliza mkataba wa miaka miwili wa mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kurudishwa majumbani.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiao wa (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Ilonda wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu nafasi za kujiunga na Jeshi hilo.
Ilonda amesema kuwa nafasi hizo zinawahusu vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha 4 na cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.
Amesema kuwa nafasi hizo haziwahusu vijana ambao bado wapo katika kambi mbalimbali za JKT kwa sasa bali zinawahusu wale ambao tayari wamemaliza mikataba yao ya mafunzo ya miaka miwili na kurudishwa majumbani na wenye vigezo vilivyotajwa vya kuomba nafasi hizo.
"Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya Jeshi hilo Dodoma kwanzia leo tarehe 9 Machi hadi tarehe 20 Machi 2023 yakiwa na viambatanisho kama vile nakala ya kitambulisho cha Taifa au namba ya Nida, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya muombaji,"amesema Ilonda.
Aidha amewataka wananchi kuwa makini na matapeli kwani kumekuwa na tabia ya kuibuka matapeli pindi matangazo hayo ya nafasi ya kujiunga na Jeshi hilo zinapotangazwa.
No comments:
Post a Comment