Sunday, October 4, 2026

NYONGO KUKABILI MIGOGORO YA ARDHI KWA MBINU MPYA

MKUU wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amekuja na mkakati kabambe wa kupambana na migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kituo cha uuzaji ardhi badala ya kutumia matapeli.

Nyongo aliyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa hafla ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Kibiti Luteni Kanali Fortunatus Kipeta.

Alisema kuwa migogoro ya ardhi ndani ya Mkoa imekuwa ni mingi sana hivyo lazima kuja na njia mbadala ya kudhibiti changamoto hiyo ili kupunguza migogoro hiyo.

"Njia mojawapo ni kuwa na kituo cha uuzaji ardhi ambapo mtu akitaka kuuza ardhi anapeleka taarifa na kununua ardhi atakwenda kwenye kituo hicho na kupata taarifa na kununua,"alisema Nyongo.

 Alisema kuwa kituo hicho kitakuwa na vitengo vyote vinavyohusiana na uuzaji na umilikaji wa ardhi ambapo taratibu zote zitafuatwa na mtu akiuziwa kiwanja hakitakuwa na changamoto yoyote.

"Matapeli wote wasakwe mmoja baada ya mwingine kwani hatutaki migogoro ya ardhi na wanauchafua Mkoa wetu kwani hawa wamewaibia hadi wawekezaji hali ambayo inaleta taswira mbaya na kuchelewesha maendeleo,"alisema Nyongo.

Aliwataka wakuu wa wilaya na timu za usalama kutatua migogoro ya ardhi ambayo baadhi inasababishwa na watumishi wa serikali kwa kushirikiana na genge linalojihisisha na kuuza ardhi za watu hivyo watenge siku maalumu kusikiliza kero hizo.

"Pia wakuu wa wilaya tatueni changamoto mapema msisubiri wananchi waje kulalamika kwa viongozi wa ngazi za juu na mzingatie weledi na utaalam na ushirikiano na hakikisheni mnaongeza mapato pia anzeni maandalizi ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kidato cha kwanza 2028 wanafunzi watakuwa wengi sana,"alisema Nyongo.

Alimtaka Mkuu huyo wa Wilaya ya Kibiti kutumia fursa kuhamasisha uwekezaji kwani wilaya hiyo haina viwanda kupitia sekta za kilimo uvuvi na kutumia bomba la gesi linalopita kwenye wilaya hiyo.

Naye Mkuu mpya wa Wilaya ya Kibiti Luteni Kanali Fortunatus Kipeta alisema kuwa atawatumikia wananchi kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu kwani cheo ni dhamana pia kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kipeta alisema kuwa atahakikisha anahamasisha amani kwa kushirikiana na makundi mbalimbali wakiwemo wazee vijana wanawake na watu wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment