KIWANDA cha Lake chakubali kuondoa mabaki ya kemikali ya salfa inayolalamikiwa na wananchi kuleta athari za kiafya eneo la Matunda Mtaa wa Lulanzi Kata ya Picha ya Ndege Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Kiwanda hicho kiliridhia kuondoa mabaki hayo baada ya wananchi kulalamika wakati wa ziara ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo kutembelea kiwanda hicho ambacho kiko kwenye hatua za ujenzi.
Mawazo amesema kuwa ili kuepuka athari za kiafya ambazo zinaweza kujitokeza hasa katika kuelekea mvua kubwa za Elnino zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni kuna haja ya kiwanda hicho kutoa mabaki ya kemikali hizo hadi ifikapo Oktoba 17.
"Wananchi hapa wanalalamika kuwa kuna kemikali ambazo zina athari kiafya hivyo fanyeni kila njia kuziondoa ili zisilete madhara hasa wakati wa mvua ndipo zinaposambaa kwenye makazi ya wananchi,"amesema Mawazo.
Alisema serikali inahitaji uwekezaji lakini uzingatie afya za watu kwani endapo kemikali hizo zitaendekea kubaki hapo na kusambaa kwenye makazi ya watu zinaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi.
Moja ya wananchi wa eneo hilo la Matunda Yusuph Mohamed amesema kuwa kemikali hiyo imemwathiri kwani nyumba yake imepasuka migomba imekauka na ametoa taarifa kwa uongozi lakini hakuna msaada wowote.
Naye Frida Kitundu amesema kuwa hivi karibuni kiwanda hicho kilitoa kemikali hiyo lakini hawakuimaliza kwani ilikuwa nyingi sana na hutiririka hasa kipindi cha mvua na ni changamoto hasa kwa watoto ambao hucheza bila ya tahadhari.
Kitundu amesema ili kuwe na usalama waitoe kemikali hiyo kwa kuchimba na kuweka udongo mwingine pale watakapokuwa wameitoa na wasitiririshe maji toka kwenye kiwanda hicho bali wawe na mfumo wa kuyatibu maji.
Akijibu malalamiko hayo Msimamizi wa ulinzi wa kiwanda hicho cha Lake Rajab Masanja amesema kuwa watafanya itaratibu wa kuondoa mabaki hayo ya kemikali hiyo ili kuondoa changamoto hiyo.
Masanja amesema kuwa kemikali hiyo ilikuwa inatumika zamani lakini kwa sasa haipo tena na wamekuwa wakiitoa na watahakikisha hadi muda uliopangwa watakuwa wamekamilisha zoezi hilo.

No comments:
Post a Comment