KIWANDA cha Qounquer Investment Company Ltd cha Kibaha kimetoa mifuko 100 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa Bweni la Shule ya Sekondari Mwambisi Kongowe.
Akitoa shukrani Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo aliyetembelea kiwanda hicho amesema kuwa saruji hiyo itasaidia ujenzi wa bweni hilo ambalo litakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mawazo amesema kuwa wanafunzi wengi wa shule hiyo wanaishi mbali hivyo kuwa na changamoto mbalimbali wakati wa kwenda shule au wakirudi nyumbani.
"Wawekezaji wanapaswa kuichangia jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo kwani hapa wanaunga mkono serikali kwenye sekta ya elimu hivyo kuwawezesha wanafunzi kupata elimu kwenye mazingira rafiki,"amesema Mawazo.
Amesema kuwa sheria inawataka wawekezaji kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo kwa jamii inayozunguka uwekezaji uliopo.
Kwa upande wake Ofisa Masoko na Mahusiano wa kiwanda hicho kinachojihusisha na utengenezaji wa Tishu Robert Bakley amesema kuwa wameamua kuunga mkono serikali ili kuboresha ushirikiano uliopo.
Bakley amesema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali na kwa changamoto ambazo zimesemwa na wananchi jirani na kiwanda hicho watazirekebisha baada ya wiki moja.
Amesema kuwa pia wataachana na matumizi ya kuni na kutumia nishati safi ili kuunga mkono jitihada za serikali za kutaka matumizi ya nishati safi.
Naye moja ya wananchi waliojirani na kiwanda hicho Samwel Raphael amesema kuwa kiwanda hicho kinapaswa kuweka mifumo mizuri ya maji ili kuepukana na adha ya maji yanayotoka kiwandani hapo yasilete athari.
Saada Almas amesema kuwa kutokana na changamoto za maji yanayotoka kiwandani hapo lazima kiwanda kichukue hatua kurekebisha hali hiyo.

No comments:
Post a Comment