HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imekipongeza kiwanda cha KEDS kikichopo Picha ya Ndege kwa kutekeleza agizo la kusafisha mtaro wa maji yanayotoka kiwandani hapo na kuondoa kero ya majitaka kwenda kwenye makazi ya watu.
Aidha kimepongezwa kwa kuweza kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania zaidi ya 500 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuzalisha ajira kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho kinachojihusisha na uzalishaji wa sabuni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Dk Nicas Mawazo amesema kiwanda hicho kilikuwa kinatiririsha maji taka ambayo yalikuwa ni kero kwa wananchi wa eneo la Matunda Kata ya Picha ya Ndege.
Mawazo amesema kuwa kiwanda hicho kimetekeleza agizo walilopewa la kutakiwa kusafisha mtaro huo ili maji hayo yasiende kwenye makazi ya watu na kuondoa kero kwa wananchi na kuepusha athari za kiafya.
"Tunawapongeza kwa kutekeleza agizo mlilopewa tulipotembelea changamoto ilikuwa ni kubwa lakini tumeona kazi mliyoifanya hasa tukielekea kipindi cha mvua kubwa za Elnino pia tumeambiwa kuna eneo limebaki kama mita 300 fanyeni mpango msafishe na kuboresha ili mvua zikianza maji yapite na yasielekee kwenye makazi ya wananchi,"amesema Mawazo.
Katika hatua nyingine ameomba kiwanda hicho kisaidie ukarabati wa mabati ya Shule ya Msingi Lulanzi ambayo iko kwenye hali mbaya licha ya kuwa shule hiyo ni moja ya shule zinazoongoza kwa kuwa na ufaulu mkubwa kwenye Manispaa hiyo.
Mawazo amesema ni utaratibu wa kisheria wawekezaji kusaidia jamii ambayo iko jirani na uwekezaji hivyo waangalie namna ya kusaidia shule hiyo kwani mvua kubwa zitakaponyesha kunaweza kutokea changamoto kubwa ya usomaji kwa wanafunzi.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole unakopita mtaro huo amesema kuwa mvua inaponyesha maji yamekuwa yakiingia kwenye makazi ya watu hivyo kwa kusafishwa mtaro huo kutasidia kuondoa changamoto hiyo.
Moja ya wananchi wa Mtaa huo Farid Hamis amesema kuwa eneo hilo lililobaki walisafishe kwani mvua kidogo ikinyesha maji yabaelekea kwenye nyumba zao hivyo hofu yao mvua za Elnino zikinyesha changamoto itakuwa kubwa sana.
Kwa upande wake Meneja Biashara wa kiwanda hicho Derick Doedatus amesema kuwa eneo lililobaki kusafishwa lilishindikana baada ya mmoja ya wananchi kugoma kuwa ardhi yake inapunguzwa kutokana na mtaro huo kutanuliwa ili maji yapite kwa urahisi hata hivyo watamalizia sehemu iliyobakia.
Deodatus amesema kuwa ombi la kusaidia Shule ya Msingi Lulanzi wamelichukua na kutaka uongozi wa shule hiyo kuandikia kiwanda ili kiweze kusaidia changamoto hiyo ya mabati.

No comments:
Post a Comment