MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo ametoa mifuko 150 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule ya awali na msingi ya Finest
Aliahidi kutoa saruji hiyo wakati wa mahafali ya wanafunzi wa awali wa shule hiyo iliyopo Kata ya Mkuza Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Mawazo amesema kuwa elimu kwa watoto ni kitu cha msingi sana hivyo lazima ipewe uzito wa aina yake kwa watu kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu.
Amesema kuwa anawapongeza wawekezaji kwenye elimu kwani zamani sekta ya elimu ilikuwa inawekezwa na taasisi kubwa lakini kwa sasa wanawekeza hata vijana.
"Elimu ni kila kitu hivyo lazima tuwekeze kwenye elimu kwa kusomesha watoto wetu na hakuna namna lazima tuwekeze ili watoto wasome hadi chuo kikuu kwani elimu ni kitu cha thamani kubwa,"amesema Mawazo.
Aidha amesema kuwa wazazi lazima wajinyime ili watoto waweze kupata elimu huku nchi ikielekea kwenye Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayotaka kila mtoto apate elimu bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule hiyo Abubakar Allawi amesema kuwa moja ya changamoto ni miundombinu ya barabara pamoja majengo.
Allawi amesema kuwa lengo la kuanzishwa shule hiyo ni kutoa elimu bora kwa gharama nafuu ili vijana wa Kibaha wawe na elimu bora itakayoendana na wakati.

No comments:
Post a Comment