Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo wakati wa hafla ya kuanza kwa ujenzi wa miradi miwili ya upanuzi wa kiwanda hicho.
Nyongo alisema kuwa upanuzi wa kiwanda hicho utaongeza ajira mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa Mkoa.
Alisema kuwa miradi hiyo inahusisha mstari wa tatu wa uzalishaji wa vigae na awamu ya pili ya uzalishaji wa bidhaa za kauri inayotarajiwa kukamilika Juni 2027.
"Baada ya upanuzi uwezo wa uzalishaji utaongezeka hadi mita za mraba 180,000 za vigae na zaidi ya vipande 200,000 vya bidhaa za kauri kwa siku huku uwekezaji wa kampuni nchini ukitarajiwa kufikia dola za Marekani milioni 200,"alisema Nyongo.
Alisema kuwa vijana wanapaswa kutumia fursa za ajira na wananchi kulinda mali za wawekezaji na viwanda ili kuendelea kuchangia maendeleo ya wananchi.
"Serikali itawasiliana na mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za tozo za vigae katika masoko ya kikanda ili kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji zaidi,"alisema Nyongo.
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Xiaoming Xie alisema kuwa upanuzi huo unatarajiwa kuongeza ajira za moja kwa moja hadi kufikia takribani 4,000, ikijumuisha ajira mpya 1,000 pamoja na fursa nyingine 15,000 zisizo za moja kwa moja.
Xie alisema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya malighafi zinazotumika kiwandani hapo zinapatikana hapa nchini huku kampuni ikiendelea kukuza bidhaa za Made in Tanzania na kuchangia maendeleo ya jamii.

No comments:
Post a Comment