MEYA wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo ametoa siku 14 kwa kiwanda cha kuchakata plastiki cha A-One Product Brothers Ltd kilichopo Visiga Madafu Kibaha kurekebisha mfumo wa majitaka ili yasiende kwenye vyanzo vya maji.
Dk Mawazo alitoa maelekezo hayo wakati alipokuwa na ziara ya kutembelea viwanda kuangalia changamoto mbalimbali zinazokabili viwanda hivyo.
Amesema kuwa serikali inahitaji wawekezaji lakini wanapaswa wanapaswa kufuata taratibu ili kuepuka athari zikiwemo za kimazingira.
"Tumetembelea kiwanda baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya majataka ambayo yanakwenda kwenye vyanzo vya maji ambayo yanatumiwa na wananchi,"amesema Mawazo.
Aidha amesema kuwa kiwanda hicho kilitakiwa kirekebishe mifumo hiyo lakini hakijatekeleza hivyo kitaandikiwa ilani ya kutakiwa kufanya marekebisho hayo.
Kwa upande wake Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Bayson Bogoza amesema kuwa kila kiwanda kinapaswa kuwa na mifumo ya usafishaji maji taka.
Uongozi wa kiwanda hicho kupitia meneja wake ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Jamal amesema kuwa wamepokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi kwa muda huo uliopangwa.
Wakati huo huo ametoa siku saba kwa kiwanda cha kutengeneza betri cha China Boda kilichopo Machinjioni Kibaha kuhakikisha wafanyakazi wake wanavaa vifaa vya kujikinga kiafya na usalama kazini.
Mawazo amesema kuwa baada ya kutembelea kiwanda hicho ameshangazwa kuona wafanyakazi hao kutovaa vifaa vya kujikinga kiusalama hali ambayo ni hatari kiafya.
Amesema kuwa suala la afya kwa wafanyakazi ni muhimu sana kwani bila ya kuzingatia masuala ya kiafya ufanyaji kazi utakuwa na changamoto.
"Taifa linahitaji watu wake kuwa na afya njema ili kuongeza uwajibikaji lakini kama wafanyakazi watakuwa hawana afya njema itapunguza ufanisi katika uzalishaji,"amesema Mawazo.
Naye meneja rasilimali watu wa kiwanda hicho Anna Edward amesema kuwa ndani ya wiki moja watahakikisha vifaa hivyo vinapatikana ili kuendana na matakwa ya kisheria.

No comments:
Post a Comment