Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amewahimiza wananchi kujiunga na Mpango wa Afya kwa Wote ili kulinda familia zao dhidi ya gharama kubwa za matibabu. Wito huo ameutoa Oktoba 22, 2026, wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa mpango huo mkoani Pwani.
Amesema awamu hiyo inahusisha usajili wa kaya za wananchi wasio na uwezo wa kifedha pamoja na zile zenye uwezo, kwa mchango wa Shilingi 150,000 kwa kaya yenye watu wasiozidi sita. Mpango huo utamwezesha mwananchi kupata matibabu katika vituo vya afya ndani na nje ya Mkoa wa Pwani.
Mhe. Nyongo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia utekelezaji wa mpango huo unaolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu bila vikwazo vya kifedha. Ameeleza kuwa tangu Februari 2026, Serikali imeanza kugharamia mpango huo kwa makundi maalumu yenye uhitaji, yakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu.
Aidha, amewaagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata elimu na fursa za usajili katika vijiji, mitaa na kata zote, huku NHIF ikitakiwa kuweka mawakala wa kutosha. Pia, amesisitiza tathmini ya usajili baada ya siku 10, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, na kuhakikisha kila mwananchi aliyejiunga anapata matibabu bila vikwazo visivyo halali.

No comments:
Post a Comment