MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ndg. Ramadhan Kimara, amesisitiza ukamilishaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati wakati akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkupuka yenye thamani ya Sh milioni 528 na Kiwanda cha Samaki cha Nyamisati.
Ramadhan Kimara amefanya ziara hiyo leo, Oktoba 12, 2026, wilayani Kibiti, akianza na ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo iliyopo Kijiji cha Mkupuka.
Akiwa eneo la ujenzi, amezungumza na fundi pamoja na msimamizi wa ghala la vifaa vya ujenzi, akiwataka kuhakikisha vifaa vinatumika kwa usahihi na kwa malengo yaliyokusudiwa na kumtaka fundi kukamilisha kazi ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.
Aidha, amemtaka Mhandisi wa mradi kufika eneo la ujenzi mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya kazi na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Mjulisheni Mhandisi wa mradi ahakikishe muda wote anafika katika eneo la ujenzi ili kusiwe na changamoto zozote katika ujenzi huu,” alisema Kimara.
Katika ziara hiyo, Ramadhan Kimara pia ameshiriki na mafundi katika ujenzi wa vyoo vya wanafunzi kwa kubeba matofali na kuyasogeza eneo la ujenzi.
Baada ya kukagua mradi huo, Kimara alielekea Kijiji cha Nyamisati, Kata ya Salale, kutembelea Kiwanda cha Samaki na kukagua miundombinu iliyopo pamoja na kubaini changamoto zinazokikabili.
Alijionea hali ya kiwanda na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuwezesha uwekezaji huo kuanza au kuimarisha shughuli za uzalishaji, kwa lengo la kuongeza mapato ya Halmashauri na kuchochea shughuli za kiuchumi wilayani Kibiti.
No comments:
Post a Comment