MKURUGENZI mpya wa Halmashauri ya Kibaha Warda Maulid amekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Dk Rogers Shemwelekwa.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Idara za Halmashauri, viongozi wa chama na wa taasisi zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo.
Maulid amesema kuwa anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa majukumu mapya ndani ya Manispaa ya Kibaha.
Amesema amekuja Kibaha kuendeleza pale ambapo Mkurugenzi aliyepita ameyafanya na ameahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu mapya aliyopewa na Rais.
"Naomba ushirikiano kutoka kwa wakuu wa Idara , ofisi ya Mkuu wa Wilaya, viongozi wa dini na viongozi wa Taasisi mbalimbali ili kwa pamoja tuweze kuleta maendeleo kwa wananchi,"amesema Maulid.
Kwa upande wake Dk Shemwelekwa amesema kuwa analishukuru baraza la madiwani kwa ushirikiano alioupata kutoka kwao katika kipindi chote viongozi wa chama cha mapinduzi na wakuu wa taasisi mbalimbali ambapo waliweza kushirikiana kwa moyo mmoja.
Shemwelekwa amesema kuwa aliweza kuboresha Manispaa ya Kibaha kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuweza kujenga miradi ya kimkakati kupitia mapato ya ndani na tayari kuna miradi imekamilika na kuna mingine inaendelea na ujenzi.
Amesema kuwa hadi kufikia tarehe 30 Septemba tayari makusanyo yameshafikia asilimia 50 na ikifika mwezi Desemba makusanyo yatakuwa yamefika asilimia 100 na miezi iliyobaki ni kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo zienda kujenga miradi ya kimakati na kuwasogezea huduma karibu wananchi.
Naye Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma amempongeza Dk Rogers Shemwelekwa kwa mazuri yote aliyoyafanya ndani ya Manispaa ya Kibaha na wanamtakia majukumu mema huko aendako.
Mruma amesema kuwa Dk Shemwelekwa ameweza kuwa na ushirikiano mzuri na Baraza la madiwani na wakuu wa idara jambo ambalo liliweza kufanikisha yale mazuri yote yaliyofanyika kwa kipindi kifupi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka amesema kuwa anampongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Maulid kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais wanamkaribisha na watampa ushirikiano katika kila hatua.
Nyamka amesema kuwa wanaamini watapata ushirikiano wa kutosha kkwa Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa Ilani kutoka kwa Mkurugenzi mpya wa Manispaa.

No comments:
Post a Comment