Thursday, October 8, 2026

MZABUNI WA USAFI SOKO LA LOLIONDO APEWA SIKU TATU SOKO LISIWE NA UCHAFU

MZABUNI wa usafi wa soko la Loliondo amepewa siku tatu kuhakikisha anaondoa uchafu uliopo sokoni hapo na kutoa takataka kwa wakati ili kuliweka soko hilo kwenye hali ya usafi.


Agizo hilo limetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo alipotembelea soko hilo kusikiliza kero na changamoto za soko na kuzitatua.

Mawazo memwagiza mzabuni huyo Sosamy kuhakikisha soko hilo linakuwa safi na kuacha kurundika uchafu ambao unakaa muda mrefu na kuwa kero kwa wananchi wanaohudumiwa na soko hilo pamoja na wafanyabiashara hao.

Amesema kuwa amepata malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hilo kwani mzabuni huyo amekuwa akichelewesha kuondoa takataka kwa wakati hivyo anatoa siku tatu soko hilo lisiwe na uchafu ikiwa ni pamoja na kusafisha mitaro ya soko hilo.

Naye Mwenyekiti wa soko hilo Mohamed Mnembwe amesema kuwa wamekuwa wakimhimiza mzabuni huyo kutoa takataka kwa wakati lakini ameshindwa kutekeleza na kulundika takataka hivyo kusababisha kero sokoni hapo.

Nao baadhi ya wafanyabiashara Wastara Kilindo na Sheba Kalage wamesema kuwa uchafu huo unaozalishwa ni mwingi na unapaswa kutolewa kwa wakati ili kuondoa kero za uchafu.

Ziara hiyo ya Mstahiki Meya wa Manispaa ikiwa na lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya usafi na barabara ili kukabilina na mvua za Elnino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.


No comments:

Post a Comment