JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamsaka Mkazi wa Kimara Dar es Salaam Seif Ally kwa tuhuma za kumuua mtoto wa kambo (10) kwa madai ya mama wa marehemu kumkataa.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Polisi Mkoani humo Salim Morcase amesema kuwa mtuhumiwa alitekeleza mauaji hayo baada ya kukataliwa na kuhusisha tukio hilo na wivu wa kimapenzi.
Mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Lugoba Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo alikuwa akiishi na bibi yake.
Morcase amesema kuwa taarifa zinaeleza kuwa usiku wa Oktoba 9 2026 mtuhumiwa alifika katika Kijiji cha Mboga alipokuwa akiishi mtoto na bibi yake na kumchukua mtoto huyo na kwenda naye kusikofahamika.
"lipofika tarehe 10 Oktoba 2026 mtuhumiwa huyo alimtumia bibi wa mtoto huyo ujumbe wa maneno kwenye simu yake ya mkononi akimuelekeza mahali ulipo mwili wa mjukuu wake na kumtaka kama akimtaka mjukuu wake kwenda kuchukua mwili wake katika Kijiji cha Rodi Chini Kata ya Lugoba Wilaya ya Kipolisi Chalinze,"amesema Morcase.
Amesema kuwa baada ya kupokea ujumbe huo bibi wa mtoto huyo alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ambalo lilifika eneo la tukio na kukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa umetelekezwa kichakani na kufunikwa kwa majani ukiwa unatokwa na damu mdomoni.
"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi baada ya mtuhumiwa kukataliwa na mama wa mtoto huyo ambaye waliachana miezi miwili iliyopita na mama huyo kukataa kurudiana naye baada ya kuachana kwao,"amesema Morcase.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo ili taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake kuhusiana na tukio hilo.
mwisho.

No comments:
Post a Comment