Sunday, October 18, 2026

MKURUGENZI MANISPAA YA KIBAHA AKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Bi. Warda Abeid Maulid, Oktoba 17, 2026, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo, ikiwemo Misugusugu, Kongowe, Picha ya Ndege, Tangini na Tumbi.

Katika ziara hiyo, Bi. Maulid ametembelea na kukagua mradi wa maegesho ya malori, vituo vya kibiashara vya Kongowe na Kwa Mbonde, kituo cha biashara cha ATN kilichopo Picha ya Ndege, pamoja na miradi ya TACTIC inayohusisha ujenzi wa barabara na Soko la Loliondo. Aidha, ametembelea jengo la utawala la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha.

Lengo la ziara hiyo ni kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, kutathmini hatua iliyofikiwa na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili ianze kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Manispaa ya Kibaha.

Akihitimisha ziara hiyo, Mkurugenzi amewataka wasimamizi na wakandarasi wa miradi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mikataba na muda uliopangwa ili miradi ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Akiwa katika Soko la Loliondo, Bi. Maulid amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi kwa juhudi zaidi, ikiwemo kutumia muda wa ziada inapowezekana, ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo. Amesisitiza kuwa kukamilika kwa soko na barabara kutarahisisha shughuli za biashara na kuwawezesha wananchi kupata huduma bora katika mazingira yaliyoboreshwa.

Miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha za kuboresha miundombinu, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment