WAZIRI wa Katiba na Sheria Abdala Ulega amewataka wananchi kujitokeza kupata huduma za Msaada wa Kisheria kutoka kwa wataalam wa sheria.
Aliyasema hayo stendi ya zamani ya Maili Moja Kibaha wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia awamu ya pili kwa Mkoa wa Pwani.
Ulega alisema Msaada wa kisheria ni kwa watu wote bila ya kujali uwezo wa mtu na unatolewa bure hasa kwa makundi yakiwemo ya wanawake watoto watu wenye ulemavu na wale wasio na uwezo.
"Msaada wa kisheria utasaidia wanyonge wapate haki zao kwa wakati hili ni jambo la kimungu na kusaidia wanyonge na mkakati huu maalum ni uendelevu,"alisema Ulega.
Alisema msaada wa kisheria unasaidia watu walio pembezoni na wasio na uwezo hivyo ni muhimu sana wananchi wakatumia fursa hiyo ambayo inatolewa bure.
"Haya ni maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutaka wananchi wapate haki zao za kimsingi kwani wananchi wakipata haki watadumisha amani,"alisema Ulega.
Alisema kuwa serikali imeweka mazingira mazuri kwenye suala la utoaji haki kwa kutoa msaada wa kisheria na elimu ya sheria ili wananchi wapate haki.
"Kutokana na uhaba wa mawakili tunaandaa utaratibu wa mawakili wa serikali kwenye wilaya kuhudumia wananchi ili kuhakikisha watu wanapata haki zao,"alisema Ulega.
Aidha alisema kuwa Msaada wa kisheria umefanikisha watu kupata haki zao kwani gharama za watu kumudu kulipa wanasheria imekuwa changamoto.
"Hii ni ibaada kuwasaidia wanyonge ambayo ikitumika vizuri itafanya watu wapate haki zao kwa wakati hali itakayosaidia kila upande kupata haki zake,"alisema Ulega.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo alihakikishia wananchi upatikanaji wa msaada wa kisheria katika Halmashauri zote tisa za mkoa huo kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Nyongo alisema kuwa wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na fursa hiyo inayotolewa bila malipo ikiwemo kupata elimu ya kisheria na ushauri kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu.
Kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa sheria kuwawezesha wananchi kutetea haki zao na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wote.

No comments:
Post a Comment