WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki amekabidhi magari 43 kwa Watendaji wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika ngazi ya Makao Makuu, Mikoa na Makatibu Tawala Wasaidizi wanaoshughulika na Miuondombinu katika ngazi za Mikoa.
Makabidhiano hayo yamefanyika Julai 05, 2023 Makao Makuu ya TARURA - Mtumba Dodoma kwa watendaji hao kwa ajili ya kuwawezesha kuboresha utendaji kazi wao.
Waziri Kairuki amesema magari 30 kati ya 43 ni kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) makao makuu na mikoa na magari 13 ni kwa ajili ya ofisi za wakuu wa mikoa kwa ajili ya usimamizi wa kazi za miundombinu.
Amesema lengo kuu kukabidhi magari haya kwa TARURA na mikoa ni kuwawezesha kuboresha utendaji kazi, hususan katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara."
“Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kuhakikisha kuwa inatoa huduma bora kwa wananchi, imeendelea kuwezesha taasisi za umma, hususan Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini, kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ili kuimarisha utendaji kazi na usimamizi wa miradi”
Aidha, Waziri Kairuki amesema hadi sasa wakala imefanya manunuzi ya magari 270, ambapo magari hayo yamekuwa yakiwasili kwa vipindi tofauti, na kukabidhiwa kwa wahusika na hivyo kufanya magari yaliyokabidhiwa kuwa 241, tangu wakala ulipoanza ununuzi wa magari Julai 2017 hadi Juni 2023.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuimarisha ubia baina ya wananchi na Serikali.
“magari haya yatasaidia kurahisisha huduma ya usafiri kwa watendaji wa TARURA na makatibu tawala wasaidizi sehemu ya miundombinu katika kusimamia, kuratibu na kufuatilia shughuli ujenzi katika mikoa” amesema Waziri Kairuki
Kadhalika, Waziri Kairuki amesema magari hayo yatagawiwa kwenye Ofisi za TARURA na Ofisi za Sekretatieti za Mikoa zenye changamoto na uhitaji zaidi wa magari kwa sasa, na zenye maeneo makubwa ya kusimamia.
Amesema Sekretarieti za mikoa zitakazopata magari awamu hii ni Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Mara, Lindi, Dodoma, Tabora na Tanga.
Ameagiza magari yatumike kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Serikali, ili yalete tija katika kuboresha huduma kwa wananchi ikiwemo kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kijamii na kiuchumi, kutokana na kuwa na miundombinu bora, na sio kutumika katika matumizi binafsi kinyume na taratibu.
No comments:
Post a Comment