KATIKA kuhakikisha wafanyabiashara wanaondokana na changamoto mbalimbali Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imejipanga kuhakikisha inakabili kero na kuzifikisha sehemu husika.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe wakati wa mkutano wa wafanyabiashara mkoani Tanga.
Amewataka wafanyabiashara hao kuungana na kuwa na sauti ya pamoja katika kuhakikisha wanajenga jumuiya yao kwa kutetea masilahi ya biashara zao.
Livembe amesema kuwa umoja wa wafanyabiashara unasaidia katika kutatua kero na kuisaidia serikali katika kutatua changamoto za wafanyabiashara pamoja na kuundwa kwa sera bora ya biashara.
"Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ipo katika kusaidia na kutatua kero za wafanyabiashara kwa makundi siyo kwa mtu mmoja mmoja ndiyo maana waliunda kamati maalum ambayo lengo lake lilikuwa ni kukusanya na kuchakata na kuwasilisha kwa serikali," amesema Livembe.
Awali katibu wa JWT Mkoa wa Tanga Ismail Masod amesema kuwa hadi sasa bei ya vitenge imeshuka ambapo awali ilikuwa kati ya shilling milioni 200 na milioni 300 lakini kwa sasa ni shilingi milioni 60 kwa kontena ambayo hiyo ni kazi ya kamati iliyoundwa.
Masod amewataka wafanyabiashara wa Tanga watumie fursa ambazo serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeziweka kwa kuagiza mizigo China kutokana na mfumo mzuri ambao serikali wameutengeneza.
Naye Mwenyekiti wa Kariakoo Martin Mbwana amesema kuwa serikali ipo pamoja na Jumuiya hiyo hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara watambue fursa na thamani ambayo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ambayo ameitoa kwa wafanyabiashara hao.
No comments:
Post a Comment