MAOFISA Utumishi wa Halmashauri nchini wameonywa kwa kutakiwa wabadilike na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuwaondolea kero watumishi.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kikwete alisema kuwa baadhi ya maofisa Utumishi wamekuwa hawatoi haki kwa watumishi hali ambayo inasababisha malalamiko kwa watumishi na kushindwa kufanya kazi kwa moyo jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
"Maofisa Utumishi ni kama vile baba na mama kwa watoto hivyo lazima wawatendee haki lakini baadhi wanafanya mambo ambayo hayapendezi wanasemwa vibaya hatupendi kuona watumishi wanamalalamiko kila mtu atimize wajibu wake kwa weledi na ubunifu kwani watumishi ndiyo msingi wa serikali,"alisema Kikwete.
Alisema kwa upande wa watumishi aliwataka wafanye kazi kwani wao ni chachu ya maendeleo na wawe na utumishi utakaoweza kupimwa kwa kutoa huduma bora kwa wateja.
"Kuna baadhi ya watumishi wanacheza karata ofisini hii inaonyesha ni kukosa ubunifu haipendezi watu wanachangamoto nyingi wanahitaji kupatiwa huduma na nyie mliajiriwa kwa ajili yao hivyo mnapaswa kuwajibika kwa wananchi,"alisema Kikwete.
"Kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali inategemea kutumia jumla ya shilingi bilioni 10.8 kwa ajili ya Bajeti ya Mishahara kwa watumishi wa Umma katika matukio mbalimbali ya kiutumishi,"alisema Kikwete.
Alibainisha kuwa hata kwa bajeti ya nyuma ya mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali ilitegemea kutumia jumla ya shilingi bilioni 9.7 kwa ajili ya Bajeti ya Mishahara kwa watumishi wa Umma katika matukio mbalimbali ya kiutumishi hali inaoonyesha serikali inakabili changamoto za fedha za watumishi wa umma.
Naye Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa watumishi wanapaswa kuboresha utendaji kazi wao ili malengo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi yafikiwe.
Kunenge alisema kuwa endapo kila mtumishi wa umma atawajibika kwenye sehemu yake malalamiko ya wananchi hayatakuwepo hivyo lazima waongeze uwajibikaji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment