NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete ameshauri Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuvipatia fedha za mikopo za asilimia 10 vikundi vya ujasiriamali vilivyopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Kikwete ameyasema hayo kwenye Kitongoji cha Mwembebaraza kata ya Janga Mlandizi Wilayani Kibaha alipotembelea vikundi vya wajasiriamali wanaotokana na fedha za kuweka akiba na kukuza uchumi wa kaya (LE) kupitia Tasaf.
Amesema kuwa wajasiriamali watokanao na vikundi hivyo wanafanya shughuli ambazo zinaonekana na ni watunzaji wazuri wa fedha ambapo wanakopeshana wenyewe kwa wenyewe japo ni kidogo lakini manufaa yanaonekana.
"Nafikiri mkurugenzi katika zile asilimia 10 vikopesheni vikundi hivi kwani wanauaminifu mkubwa na wanatumia fedha kwa malengo ambayo yanaonekana kupitia miradi hii kuanzia ile ya uhawilishaji wa fedha, miradi ya ajira za muda na miradi ya ujenzi wa miundombinu,"alisema Kikwete.
Aidha amesema kuwa endapo fedha zitatolewa kwa vikundi hivyo fedha za serikali hazitapotea ambapo vikundi vinavyolengwa vimekuwa havirudishi fedha wanazokopeshwa lakini vikundi vya Tasaf ni waaminifu sana.
"Tasaf imekuwa mkombozi kwani imeweza kubadili maisha ya kaya lengwa kutoka chini na kuinuka kiuchumi na kuondoka kwenye hali ya chini na kuboresha maisha kama malengo ya serikali yalivyowekwa kwani mpango umetafsiriwa kwa vitendo,"alisema Kikwete.
Kwa upande wake mratibu wa Tasaf Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha akisoma taarifa ya mpango huo wa kunusuru kaya masikini Sijaona Muhunzi alisema kuwa kaya lengwa zimenufaika kupitia vikundi na mtu mmoja mmoja.
Muhunzi alisema kuwa baadhi ya walengwa wameweza kujenga nyumba, kufanya ufugaji, kilimo cha mboga mboga, kusomesha watoto na kuongeza maudhurio shuleni na kliniki ambapo ni moja ya masharti kwa familia lengwa watoto kwenda shule na kliniki kwa asilimia 100.
Naye Dalia Hassan amesema kupitia mpango huo amemsomesha mwanae ambaye kwa sasa yuko chuo kikuu anasema alianza kupewa ruzuku ya shilingi 40,000 mwaka 2012 ambapo aliingiza kwenye biashara ya karanga.
Hassan amesema kuwa fedha hizo zilimwezesha kuanza kilimo cha mpunga na pilipili vimemsaidia kumsomesha mwanae huyo na kuwataka walengwa wenzake kuwa na malengo makubwa ya kujiletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment