Wednesday, July 19, 2023

WAZALISHAJI CHUMVI WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI





WAZIRI wa Madini Dk Dotto Biteko amewatakaka wazalishaji wa chumvi nchini kuongeza uzalishaji chumvi ili kukidhi soko la ndani na la nje kutoka tani 273,000 kwa mwaka hadi tani 303,000.

Aliyasema hayo alipofanya ziara ya siku moja kutembelea kuona uzalishaji wa chumvi kwenye kampuni za Sea Salt na Stanley and Sons Ltd zilizopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.

Dk Biteko alisema kuwa uzalishaji wa chumvi utakapo ongezeka utasaidia kuongeza mapato na kutoa ajira kwa wananchi ambapo asilimia 15 ya chumvi ndiyo inayopelekwa soko la nje.

"Chumvi hiyo inatumika kwa ajili ya chakula, viwandani na kuuzwa soko la nje ambapo chumvi kutoka nje ya nchi inauzwa kwa gharama ndogo ikilinganishwa na inayozalishwa ndani kutokana na gharama za uendeshaji,"alisema Dk Biteko.

Alisema kuwa ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama mamlaka za serikali za mitaa zinapaswa kufanya marejeo ya sheria zake ndogo ili zilingane ambapo kwa sasa kila Halmashauri inatoza gharama zake.

"Serikali baada ya kuona malalamiko ya wazalishaji walifuta kodi 17 na mrabaha kutoka asilimia tatu hadi asilimia moja lengo likiwa ni kupunguza gharama za uzalishaji ili bei iwe ndogo,"alisema Dk Biteko.

Aidha alisema kuwa makampuni hayo pia yawasaidie wazalishaji wadogo kwa kununua chumvi yao ili kuongeza uzalishaji na kuwataka wazalushaji hao kutokuwa watu wa kulalamika sana juu ya tozo na kodi kwani fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kutoa huduma za maendeleo.

"Tanzania ina Pwani kubwa lakini uzalishaji wa chumvi ni mdogo licha ya kuzuia chumvi za nje ili kukuza soko la chumvi inayozalishwa hapa nchini lakini pia wazalishaji wazingatie ubora,"alisema Dk Biteko.

Naye Ofisa Madini Mkoa wa Pwani Mhandisi Ally Maganga alisema kuwa Wilaya ya Bagamoyo inazalisha chumvi tani 90,000 hadi 100,000 kwa mwaka na kuingiza kati ya shilingi milioni 300 hadi miluoni 350.

Maganga alisema kuwa kuna leseni 48 za uchimbaji chumvi huku ndogo zikiwa 46 ambapo ni 15 tu ndizo zinafanya kazi huku nyingine zikiwa hazifanyi kazi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji, soko na mazingira.

Awali Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge pia kupunguzwa gharama kwa magari yanayochukua chumvi kutozwa fedha nyingi na Hifadhi za Taifa (Tanapa) ambapo makampuni hayo kutumia barabara za hifadhi ya Saadani.

Mkenge alisema kuwa endapo baadhi ya changamoto zikiondolewa Bagamoyo inaweza kulisha chumvi nchi nzima kwani wanauwezo huo wa uzalishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya H J Stanley and Sons Richard Stanley alisema kuwa baadhi ya changamoto ni kukosekana kwa umeme, maji na ubovu wa barabara.

Stanley alisema kuwa changamoto nyingine ni uingizwaji wa chumvi toka nchi nyingine ambapo miundombinu ikiwa mizuri gharama za chumvi zitapungua na bei itashuka.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Shauri Selenda alisema kuwa kilio cha wawekezaji hao kinafanyiwa kazi kwa kuboresha miundombinu na upatikanaji wa maji na umeme na barabara.

Selenda alisema tayari miundombinu hiyo imewekwa kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha ili kuwaondolea kero wawekezaji hao.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment