Monday, July 10, 2023

TASAF YATAKIWA KUANDAA TAARIFA ZINAZOAKISI MAFANIKIO YA TASAF


NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amewataka waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwenye wilaya nchini kuandaa taarifa zinazoakisi mafanikio au changamoto ya mfuko huo.

Kikwete aliyasema hayo jana akipokea taarifa ya Tasaf kwenye mkoa wa Pwani wakati wa ziara yake aliyoanzia Halmashauri ya Mji Kibaha.

Alisema kuwa taarifa hizo zinapaswa kuwa na uchambuzi wa kina ili kuweza kujua mafanikio ya mpango huo na kama kuna changamoto serikali iweze kufanya maboresho.

"Taarifa inabidi ziakisi ili wale wanaofuzu wawe na vigezo isije wakaondolewa kwenye mpango halafu baadaye wakarudi walikotoka na walio kwenye mpango wajikwamue kiuchumi na kuboresha maisha yao,"alisema Kikwete.

Alisema kuwa baadhi ya maeneo hasa kupitia fedha za kujiinua kiuchumi ambapo wilayani Rufiji limejengwa vizuri sana na akinamama wanne wa mpango huo nao wanafanyabiashara kwenye soko hilo.

Kwa upande wake Mratibu wa Tasaf mkoa wa Pwani Roselyne Kimaro alisema kuwa Uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini (CCT) kwa kipindi cha 2023 ni shilingi bilioni 14.2 zimetolewa kwa walengwa ambapo zimesaidia walengwa kuongeza kipato.

Kimaro alisema kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini hadi kufikia Juni 2023 kaya zinazonufaika na mpango ni 35,427 kutoka 37,663 na upande wa ajira za muda mpango katika kipindi hicho zimepokelewa kiasi cha shilingi bilioni 2 ikiwa shilingi bilioni 1.4.

Alisema kuwa malipo ya ujira na ununuzi wa vifaa kiasi cha shilingi milioni 568.6 zilitolewa kwa ajili ya miradi 296 iliyoibuliwa katika vijiji 224 ambapo miradi hiyo imetekelezwa na walengwa 10,904 na mpango huo umetekelezwa kwa Halmashauri nne za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha na Kisarawe.


No comments:

Post a Comment