Sunday, July 9, 2023

VYAMA VYA SOKA VYATAKIWA KUWA NA UTAWALA BORA





VYAMA vya Soka Nchini vimetakiwa kuzingatia utawala bora ili kuhakikisha sheria miongozo na taratibu za mpira zinafuatwa ili soka liweze kuimarika na kupata timu na wachezaji bora.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkurugenzi  wa Sheria Habari na masoko kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura wakati wa semina elekezi kwa Kamati Mbalimbali za Chama Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA).

Wambura alisema kuwa utawala bora kwenye mpira unasaidia kuhakikisha mpira unachezwa kwa kuzingatia taratibu za mpira zilizowekwa na chama husika.

"Utawala bora unaonyesha kila mtu anawajibika kwa nafasi yake pasipo kuingiliana kwenye majukumu yao ya kiutendaji,"alisema Wambura.

Alisema kuwa mpira una taratibu zake hivyo ili mpira uchezwe lazima sheria zake zifuatwe kwani tofauti na hapo klabu na nchi haitaweza kuwa na timu wala wachezaji wazuri.

"Kwa sasa mambo yamebadilika tofauti na zamani ambapo kulikuwa na migogoro mingi lakini kwa kuwa mambo yanaendeshwa kwa weledi na mpira umebadilika timu zimekuwa nzuri na wachezaji wana ubora,"alisema Wambura.

Aidha alisema kuwa mpira umekuwa na hadhi kutokana na kuwekwa mifumo mizuri ambapo kila mtu anafanya kazi kwa nafasi yake na huo ndiyo utawala bora.

Kwa upande wake mwenyekiti wa KIBAFA Robert Munis alisema kuwa lengo la kuandaa semina elekezi kwa kamati hizo ni kuwaelekeza viongozi kila mmoja kujua mamlaka yake.

Munis alisema kuwa moja ya changamoto zinazojitokeza ni baadhi ya viongozi kutofahamu majukumu yao hivyo kuwa na mwingiliano kiutendaji.

Awali katibu wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Mohamed Masenga alisema kuwa wao wanasimamia wilaya ili kuhakikisha mipra unachezwa.

Masenga alisema kuwa wanakipongeza chama hicho kwa kuandaa semina hiyo na kuvitaka vyama hivyo kuandaa semina kama hizo ili kuwajengea uwezo viongozi.

No comments:

Post a Comment