Monday, July 3, 2023

MUNIS ACHAGULIWA MENYEKITI KIBAFA

CHAMA Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA) kimefanya uchaguzi wake Mkuu na kupata viongozi watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne ambapo Robert Munis amechaguliwa kuwa mwenyekiti.

Munis alishinda uchaguzi huo uliofanyika Mjini Kibaha ambapo hakuwa na mpinzani, kwa kupata kura 30 na kura moja ya hapana kati ya wapiga kura 31.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilichukuliwa na David Mramba aliyepata kura 27 nafasi ya katibu ilikwenda kwa Daud Mhina aliyepata kura 29 na katibu msaidizi ni Omary Pumzi aliyepata kura 28.

Nafasi ya mweka hazina ilikwenda kwa Laurent Shirima aliyepata kura 28, nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu kwenda Corefa ni Japhet Mbogo aliyepata kura 30, Mwakilishi wa vilabu Mohamed Mwenda aliyepata kura 28.

Mwakilishi wanawake ni Jesca Siha aliyepata kura 28 huku kamati ya utendaji ni Method Mselewa, Nasoro Shomvi na Emanuel Mbunda.

Akizungumzia mikakati yake katika kipindi cha miaka minne Munis alisema kuwa moja ya mikakati yake ni kuhakikisha Kibaha inakuwa na timu ya ligi kuu ambapo ataweka mikakati Ruvu Shooting irudi kwenye ligi hiyo baada ya kushuka daraja.

Munis alisema kuwa atahakikisha mpira wa miguu unachezwa na kupata viwanja vizuri ili kukuza vipaji vya vijana kwenye soka ili waje kuwa hazina kwa timu za mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu wa chama cha soka Mkoa wa Pwani COREFA Mohamed Masenga alisema kuwa kwa vyama ambavyo havijafanya chaguzi vifanye hivyo ili kwendana na kalenda ya vyama vikuu vya soka.

Masenga alisema anapongeza uongozi uliochaguliwa na kuwataka kuzingatia mipango na taratibu zilizopo ili soka la mkoa wa Pwani lisonge mbele.

Kwa upande wake ofisa michezo wa Halmashauri ya Mji Kibaha Burhan Tulusubya alisema kuwa uchaguzi huo ulienda vizuri kwa kuzingatia taratibu za chama hicho na sheria kwani ulikuwa wa kisheria.

Tulusubya alisema kuwa viongozi hao wasimamie maneno yao kwa kutafsiri kwa vitendo na wahamasishe vilabu navyo vifanye chaguzi ili wawe kisheria. Uchaguzi huo ulisimamiwa na makamu mwenyekiti wa uchaguzi wa KIBAFA Mabel Nasua.

No comments:

Post a Comment