MKE wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 kwa Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.
Koka alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.
Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.
"Tumieni sanaa kwa ajili ya kuelimisha jamii, kuburudisha na kufundisha ili muwe sehemu ya maendeleo ya nchi na kujinufaisha wenyewe kwa wenyewe,"alisema Koka.
Awali Rais Sanaa za Maonyesho Tanzania Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.
Henjewele alisema kuwa ili wasanii waweze kutambulika wanapaswa kujisajili ili watambulike kisheria ambapo wakijirasimisha watapata fursa mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kibaha Mjini Jumanne Kambi alimshukuru mke wa Mbunge kwa mchango wake wa kukuza sanaa kwenye Wilaya hiyo.
Kambi alisema kuwa kwa kuwa sasa wana ofisi na tayari wana wanachama 700 watahakikisha wanachama wao wanaingia mikataba yenye manufaa kwa wasanii tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanadhulumiwa haki zao.
No comments:
Post a Comment