Friday, February 10, 2023

12 WAFA 63 WAJERUHIWA AJALINI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 63 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia Alhamisi Februari 9, 2023 Wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 12 (wanaume nane , wanawake wanne) na majeruhi 63 (wanaume 40 wanawake 23).

Senyamule amesema ajali hiyo imetokea usiku Kata ya Pandambili Kijiji cha Silwa wilayani Kongwa, barabara ya Dodoma - Morogoro.

"Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkoa wa Morogoro na majeruhi wawili wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,"amesema Senyamule.

Amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa  6 usiku na imehusisha lori la mizigo lenye namba za usajili T 677 DVX na basi la abiria  la Kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 415 DPP lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam.

Akizungumza na wakazi wa Pandambili eneo ambapo ajali ilipotokea Senyamule ametoa rai kwa jamii kutii sheria bila shuruti ili kuepuka ajali. 

"Serikali ilikuwa na nia njema ya kuruhusu vyombo vya usafiri kutembea usiku, lakini sasa baadhi ya madereva wanaanza kutozingatia Sheria za usalama barabarani, tutaendelea kuwachukulia hatua kali,"amesema Senyamule.a

Pia mewatembelea majeruhi katika Hospitali ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na kutoa pole na kuwatakia uponyaji wa haraka.

Naye Mkuu wa Operesheni na Mafunzo  wa Jeshi la Polisi Kamishna Awadh Haji ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi kutaka kulipita gari la mbele yake bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na lori hilo  lililokuwa limebeba saruji.


No comments:

Post a Comment