Friday, February 3, 2023

MIAKA 46 CCM JUMUIYA YA WAZAZI BAGAMOYO YAPANDA MITI SHULENI

WAKAZI wa Chalinze wilayani Bagamoyo wametakiwa kupanda miti ili kutunza mazingira kuzuia upepo wa mara kwa mara unaoezua mapaa katika majengo yao.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji wa miti katika shule ya msingi Bwilingu Kata ya Bwilingu Chalinze Mwenyekiti wa Wazazi wilaya ya Bagamoyo Aboubakary Mlawa alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwa na utamaduni wa kupanda miti mara kwa mara na si kusubiri wakati wa sherehe ama ugeni.

Mlawa alisema kuwa kwa eneo la chalinze eneo kubwa lipo wazi kwa kutokuwa na miti kutoka na ujenzi hivyo ni muhimu sasa kila mkazi awe na utamaduni wa kupanda miti.

"Kumekuwa na matukio mengi ya upepo kuezua mapaa katika majengo ya watu binafsi sambamba na majengo ya taasisi zikiwemo shule dawa pekee kuzuia hali hii ni kupanda miti kwa wingi,"alisema Mlawa.

Alisema kuwa kama kila mtu akipanda mti mmoja katika maeneo yanayomzunguka ana hakika mazingira ya majengo yao yatakuwa na usalama.

"Wao kama Jumuiya ya Wazazi jukumu mojawapo walilopewa na Chma cha Mapinduzi ambalo pia katika dhumuni la kuwepo kwa jumuiya hiyo ni utunzaji wa nazingira hivyo ni muhimu kusimamia na kuhakikisha upandaji wa miti unakuwa endelevu,"alisema Mlawa.

Aidha alisema anaomba upandaji wa miti usiwe wakati wa ujio wa wageni ama wakati wa sherehe,zoezi la upandaji miti liwe la kila siku.

Awali Diwani wa kata ya Bwilingu Nasser Karama alisema kama Diwani alihakikisha kuwa maeneo mbalimbali ya Taasisi yanapata huduma ya maji kwa kuchimba visima vya kisasa. 

Karama alisema kuwepo kwa visima hivyo kutachochea utunzaji wa miti hiyo na uboreshaji wa mazingira.

Jumuiya wa Wazazi wilaya ya Bagamoyo katika kusherekea miaka 46 ya kuzaliwa kwake ilifanya shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji misaada mbalimbali, upandaji miti na uchangiaji wa damu. 


No comments:

Post a Comment