MTAA wa Bamba Kata ya Kongowe Wilayani Kibaha imesafisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari kwa wanafunzi wanaotoka Mtaa huo ambapo hutembea umbali wa kilometa 16 kwenda Shule ya Sekondari Mwambisi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huo Mwenyekiti wa Mtaa huo Majid Kavuta amesema kuwa tayari wana vifaa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo kwa awali madarasa manne.
Kavuta ametaja vifaa hivyo kuwa ni tofali 3,600, saruji mifuko 50, mchanga lori tatu, kokoto lori mbili na wanatafuta mdau ili awapatie nondo ambapo kila kaya inatakiwa kutoa tofali 10.
"Kutokana na wanafunzi hao kusoma mbali kunasababisha utoro na wanafunzi wa kike kurubuniwa na kujiingiza kwenye mapenzi na wale wa kiume kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na uvutaji wa bhangi,"amesema Kavuta.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kongowe Simon Mbelea amesema ujenzi huo ni kutekeleza ilani ya chama kuhakikisha watoto wanapata elimu kwenye mazingira rafiki.
Mbelwa amesema pia ni kuunga mkono jitihada za Rais DK Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta ya elimu ambapo ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu nchini.
No comments:
Post a Comment