Friday, February 3, 2023

"NIKI WA PILI" AKABIDHIWA KIJITI NA SARA MSAFIRI KUONGOZA WILAYA YA KIBAHA BAADA YA MABADILIKO YA WAKUU WA WILAYA.

MKUU mpya wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ambaye amehamishiwa hapa kutoka Wilaya ya Kisarawe amesema kuwa ili kufikia ndoto za Rais DK Samia Suluhu Hassan na matarajio ya wananchi ni kujenga timu ya pamoja.

John aliyasema hayo alipokuwa akikaribishwa Wilayani hapo na viongozi na watendaji wa taasisi na wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Mji Kibaha na kumuaga aliyekuwa mkuu wa Wilaya hiyo Sara Msafiri.

Alisema kuwa wananchi wana matarajio makubwa ya kupata maendeleo kutoka kwa viongozi hivyo anachohitaji ni ushirikiano ili kuwa na timu itakayofanya kazi kwa pamoja.

"Ndoto yangu ni kuhakikisha tunashirikiana na Rais ili ndoto za kuleta maendeleo zitimie kwa ushirikiano wetu sisi tukiwa ni viongozi,"alisema John.

Aidha alisema kuwa wananchi wanamatumaini makubwa makubwa na viongozi hivyo watazingatia vipaumbele vya Rais na vya wananchi ili kuleta maendeleo.

"Ili tufanye kazi vizuri napenda uwazi na utu ambacho ni kitu kikubwa pamoja na nidhamu na uwajibikaji haya yatatusaidia katika kufikia malengo tuliyojiwekea,"alisema John.

Kwa upande wake mkuu wa zamani wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri aliwashukuru viongozi na watendaji wa Wilaya hiyo kwa ushirikiano waliompa alipokuwa hapo na kuwatakia heri wanaoendelea na utumishi kushirikiana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala alisema kuwa watahakikisha wanashirikiana na Mkuu wa Wilaya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Makala alisema kuwa kwa kushirikiana na Mkuu huyo wa Wilaya wanaamini watakuwa na ushirikiano kufikia ndoto za wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba alisema kuwa watamapa ushirikiano mkuu mpya wa Wilaya ili kuwatumikia wananchi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alisema kuwa watashirikiana naye ili kufikia pale wanapopataka.


No comments:

Post a Comment