Thursday, February 2, 2023

WATAKIWA KUPIMA VIWANJA VIWANJA


MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ametoa mwezi mmoja kwa wananchi wa mitaa ya Lumumba na Mkombozi Kata ya Pangani Wilayani Kibaha kupima viwanja vyao ambavyo serikali ilitoa baada ya kuvamia eneo lililokuwa la Kituo cha Mitamba Kibaha.

Aidha amewataka wananchi waliovamia sehemu ya Shamba hilo kuondoka kwani wako hapo kinyume cha sheria kwani eneo hilo lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa ajili ya kuliendeleza.

Kunenge aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa mitaa hiyo kutatua migogoro ya ardhi baada ya wananchi wa mitaa hiyo kugomea zoezi upimaji ardhi wakitaka warasimishiwe eneo ambalo walipewa baada ya kulivamia.

Alisema mtu anayerasimishiwa ni yule ambaye anamiliki ardhi kihalali lakini wao walipewa tu hivyo wanapaswa kupimiwa kwa gharama ya mita za mraba shilingi kwa shilingi 1,5000.

"Natoa mwezi mmoja kwa wananchi wote kwenye mitaa hiyo kupima ardhi yao ili wamiliki kihalali na malipo yalipunguzwa kutoka 2,500 hadi 1,500 kwa mita za mraba baada ya wengi kulalamika kuwa hawana uwezo,"alisema Kunenge.

Alibainisha kuwa eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na iliyokuwa Wizara ya Kilimo na Mifugo wakati huo ambapo watu walilivamia na Wizara ilibidi ilimege na kuwaachia wananchi sehemu mwaka 2012.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alisema kuwa walitoa matangazo ya wananchi kupima viwanja lakini mwitikio ukawa ni mdogo.

Munde alisema kuwa kutokana na hali ya ugumu wa kupima maeneo hayo wakitaka wayarasimishe hivyo kwa mwezi huo mmoja wanaamini watu watajitokeza kupima maeneo yao 

Shamba hilo la Mitamba lilianzishwa mwaka 1982 na 1983 na Wizara ya Kilimo na Mifugo wakati huo kwa lengo la kutoa mafunzo na uzalishaji wa ngombe bora Mitamba lilikuwa na ukubwa wa hekari 4,000 ambapo ilitoa fidia milioni 20 kwa wananchi waliokuwa wakikaa kwenye eneo hilo wapatao 1,557.




No comments:

Post a Comment