Na Mwandishi Wetu Dodoma
BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetoa wito kwa wakulima kutokubali kurubuniwa na madalali badala yake waingie kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani ili kuuza mazao yao kulingana na bei iliyopo sokoni.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Asangye Bangu Jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo.
Bangu amesema kuwa kumekuwa na wimbi la madalali kwenda mashambani kwa wakulima na kuwarubuni na kununua kwa bei ya chini hali ambayo inawakandamiza wakulima.
"Tangu kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 2007/2008 hadi 2020/2021 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2 kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,"amesema Bangu.
Amesema bodi imeendalea na juhudi za kuboresha mfumo uliokuwepo wa kizamani wa usimamizi wa ghala ambapo kwa kushirikiana na bodi inakuja na mfumo mpya wenye kuweza kurahisisha kazi za maandalizi ya taarifa utoaji stakabadhi na udhibiti wa matukio ghalani hivyo kupunguza muda wa michakato na kuongeza ufanisi na usalama wa mzigo.
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ni taasisi chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoundwa kwa Sheria namba 10 ya 2005 na Marekebisho Kifungu 4 Sura 339 mwaka 2016 iliyopewa majukumu ikiwemo kutoa leseni kwa waendesha ghala, meneja dhamana na wakaguzi wa ghala.
Majukumu mengine ni kuchapa na kuidhinisha vitabu vya Stakabadhi za Ghala, kusajili na kuingiza taarifa za wadau muhimu wa mfumo, kuwakilisha nchi katika masuala ya taifa na kimataifa yahusuyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala pamoja na majukumu mengine kama taasisi itakavyoelekezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara.
No comments:
Post a Comment