JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia mtu mmoja mwanaume (53) ambaye jina limehifadhiwa mkulima mkazi wa Kijiji cha Ruvu Stesheni Wilaya ya Kibaha akiwa na silaha aina ya Shortgun Greener yenye namba za usajli 729 na maganda sita ya Risasi za Shortgun na unga wa baruti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa kukutwa na silaha hiyo.
Lutumo alisema kuwa mtuhumiwa huyo alishafanya tukio la mauaji huko Kisarawe na kutorokea katika kijiji cha Ruvu Stesheni Wilaya ya Kibaha.
"Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika na kuwataka watu waache kutumia silaha hizo kinyume cha sheria,"alisema Lutumo.
Katika tukio lingine ambalo lilitokea mnamo Januari 8 mwaka huu majira ya saa 06:45 mchana huko maeneo ya Msanga Sokoni Kata ya Msanga, Tarafa ya Maneromango Wilaya ya Kisarawe mtu mmoja mwanaume (47) ambaye jina lake limehifadhiwa mfanyabiashara mkazi wa Msanga Sokoni alikamatwa kwa kukutwa na Bunduki aina ya Riffle yenye namba za usajili zilizofutika.
Lutumo alisema kuwa mtuhumiwa huyo hakuwa na vibali vya umiliki wa silaha hiyo ambapo ilikamatwa wakati Polisi wakiwa kwenye misako ambayo imefanyika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Aidha alisema kuwa pia risasi sita zilikamatwa baada ya kufanya misako katika wilaya za mkoa huo kwa lengo la kudhibiti makosa ya uvunjaji, unyang’anyi wa kutumia nguvu, wizi, wizi wa mifugo, utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na matumizi ya pombe harammu ya moshi (gongo).
"Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limefanya misako na operesheni mbalimbali kuanzia tarehe 1 Januari hadi tarehe 31 Januari mwaka huu ambapo Jumla ya watuhumiwa 19 wanaume wamekamatwa,"alisema Lutumo.
Aliongeza kuwa katika misako hiyo walifanikiwa kukamata pikipiki mbili za aina tofauti, Televisheni Spika, deki, feni na meza ya Tv vyote kimoja kimoja
Viti 13 waya ya Fensi rola tatu, Gongo (Pombe ya Moshi) lita 140 na Bhangi gunia 12, Puli 57 na kete 157.
"Upelelzi wa matukio haya bado unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa hawa wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowahusu,"alisema Lutumo.
Alibainisha kuwa Jeshi la Polisi linaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zozote zinazo husiana na uhalifu na wahalifu kwa wakati kwa kuwatumia wakaguzi kata waliopo kwenye maeneo yao yote ndani ya Mkoa wa Pwani nao watazifanyia kazi kwa wakati na haraka.
No comments:
Post a Comment