Monday, February 13, 2023

REDIO ZITANGAZE HABARI ZA VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

NAIBU Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinaendelea kutangaza na kuanda makala na vipindi vinavyolenga Maeneo ya Vijijini ambako kumekuwa na usikivu mkubwa wa Redio.

Methew amesema hayo Jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani ambapo kumefanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji Tanzania.

Amesema kuwa mchango wa vyombo vya habari ni mkubwa sana hasa Redio vimekuwa vikitoa taarifa nzuri hivyo kwa sasa Redio za FM zihakikishe zinakuwa na vipindi na makala nyingi zinazogusa Jamii na Utekelezaji wa Miradi ya serikali ya awamu ya sita.

"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt  Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha inasimamia na kuboresha upatikanaji wa habari serikalini na Taasisi zake kwa umakini na haraka hivyo vyombo vya habari vina haki ya kutumia fursa hiyo viweze kuitangaza nchi iliko toka na ilipo sasa ambapo kuna Utekelezaji wa miradi mingi inayowagusa Wananchi ikiwemo afya, Elimu,maji,nishati na miundonbinu,"amesema Methew.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amepongeza vyombo vya Habari hasa Redio za Dodoma kwa kuendelea kuitangaza Dodoma ambako ndio Makao Makuu ya nchi huku akiwataka wamiliki, wahariri na Waandishi wa habari katika siku mbili wapate fursa ya kuizunguka Dodoma kuona ujenzi unaoendelea kwenye mji wa kiserikali Mtumba kunaendelea ujenzi wa majengo ya wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambapo watakuwa wamefanya utalii wa ndani  ambako serikali imetoa fedha nyingi katika Ujenzi huo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Redio cha Wapo Fm Edina Malisa ameishauri mamlaka ya Mawasiliano TCRA kuhakikisha inakuwa inavitembelea vyombo vya habari na kujadiliana changamoto mbalimbali ambazo wanazipata ili kuweza kushirikiana na serikali ili kuweza kupatia ufumbuzi na kuendana na sheria na kanuni za vyombo vya habari.

Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji Tanzania umewashirikisha wamiliki wa vyombo vya habari, wakurugenzi, wahariri na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hapa nchini ambapo Mkutano huo ni wa siku mbili.

No comments:

Post a Comment