NJOMBE YATEKELEZA ILANI YA UCHAGUZI YA (CCM) KWA VITENDO
Na Elizabeth Paulo, Njombe
MKOA wa Njombe umeendelea na utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka amebainisha Utekelezaji wa miradi hiyo katika taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa Mkoa wa Njombe katika kipindi cha mwaka mmoja Julai 2021 hadi Disemba 2022.
Mtaka amesema Mkoa wa Njombe unaendelea kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kuzingatia Ilani ya Chama ambapo na Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 na malengo ya maendeleo endelevu ya Milenia yenye lengo la kuendelea kuwatumikia wananchi na kuboresha maisha ya wananchi wote.
"Kama ilani ya chama tawala inavyoelekeza Mkoa umekusudia kusimamia na kuelekeza rasilimali zake katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya, Elimu, Maji, Umeme na Makazi vijijini na Mijini pamoja na kuleta mageuzi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kujitegema kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu kwa maendeleo ya kiuchumi,"alisema Mtaka.
Amesema serikali ya Mkoa itajikita katika mambo matatu muhimu yatakayogusa maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kufuatilia wanafunzi ambao bado hawajaripoti mashuleni huku asilimia 90 ya wanafunzi kidato cha kwanza wameripoti katika shule mbalimbali ambapo awali ilikuwa asilimia12.
"Mkoa umeanzisha mkakati wa kuwaondoa wanufaika wa Tasaf baadaya miaka mitatu hadi miaka mitano kwa kuanza na Halmashauri ya Makambako ambapo katika ziara ya Waziri wa Kilimo Bashe alitoa miche ya parachichi 20,000 yenye thamani ya shilingi millioni 100 kwa wanufaika wa Tasaf hao ambapo kila kaya imepewa miche 10,"amesema Mtaka.
Aidha amesema kuwa kutokana na kero kubwa na changamoto inayowakabili wananchi na wakazi wa mkoa huo kutozwa ushuru mara mbili kuingia stendi kuu ametoa wito kwa viongozi na wakusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kutafuta vyanzo vya mapato na kuacha mapato kero kwa wananchi.
Awali akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Deo Sanga ameupongeza uongozi wa chama tawala chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi za ujenzi wa miradi ya maendeleo katika mkoa wa Njombe.
Katika kuwainua kiuchumi Halmashauri ya Mkoa imeendelea kutoa mikopo kwa Vikundi vya akina mama, Vijana na watu wenye ulemavu ambapo jumla ya shilingi bilioni 10.6 zimekopeshwa ambapo vikundi vya wanawake ni 382 vyenye wanufaika 4,062, Vijana vikundi 237 vyenye wanufaika 1,564 pamoja na watu wenye ulemavu kwa vikundi 72 vyenye wanufaika 207.
Maadhimisho ya Miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama cha mapinduzi kwa Mkoa wa Njombe imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Pindi Chana, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Elimu na Afya Dkt Festo John Dugange, Wabunge, wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, pamoja na wananchi wa Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment