MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka Wakurugenzi na viongozi ambao nafasi zao zinatokana na uteuzi wa Rais kutofanya kazi zao kwa hofu ya kutochaguliwa kwani hiyo ni mipango ya Mungu.
Kunenge aliyasema hayo Mjini Kibaha alipokuwa akiwaapisha wakuu wapya wa Wilaya na kuwakaribisha waleo waliohamishiwa vituo vyao vya kazi na kuja kwenye mkoa huo.
Alisema kuwa hakuna sababu kwa viongozi hao kutofanya kazi kwa ufanisi kuhofia uteuzi kwani hiyo itasababisha shughuli za maendeleo kutofanyika kikamilifu.
"Wakurugenzi na wale ambao nafasi zao bado hazijafanyiwa mabadiliko na Rais fanyeni kazi mambo mengine mwachieni Mungu mbona mimi nafanya kazi zangu kama taratibu zilivyo mengine tumuachie Mungu yeye ndiye anayejua,"alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa kuchaguliwa hiyo ni mipango ya Mungu hivyo kila mtu afanye kazi kwa mujibu wa sheria msihofie uteuzi kwani kazi za mtu ndiye zitakazomfanya achaguliwe tena.
"Yawezekana unaangaliwa hivyo ukifanya kazi chini ya kiwango unaweza ukajiharibia ni vema ukaendekea kuwajibika bila kujali mbele kutakuwa na nini kwani hayo ni majaaliwa,"alisema Kunenge.
Aliwataka viongozi hao ambao nafasi zao zinatokana na uteuzi wa Rais kutatua changamoto za wananchi kwani ndiyo wajibu wao na wamewekwa hapo kutokana na uwezo wao.
No comments:
Post a Comment