Tuesday, January 31, 2023

HESHIMUNI VIAPO VYENU

VIONGOZI WATAKIWA KUHESHIMU VIAPO VYAO.



Na Elizabeth Paulo,Dodoma

WAKUU wa wilaya wapya walioteuliwa wametakiwa kuheshimu na kuviishi viapo vyao walivyoviapa kwa uadilifu na uaminifu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. 

Katibu  Msaidizi  wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya kati Dodoma Bibi Jasmini Awadhi alitoa kauli hiyo alipokuwa akimwapisha Mkuu wa wilaya ya Chemba Gelard Mongela  katika hafla fupi iliyofanyika  katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma.

Awadhi aliisema kuwa wakuu hao wa Wilaya wahakikishe wanajitoa kutumikia viapo walivyoapa mbele na kuviweka katika kumbukumbu zao za kila siku ili viwasidie kuyakumbuka yale yote yaliyoelezwa katika viapo hivyo wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Katika hatua nyingine  alimpongeza Mkuu wa wilaya ya Chemba  kwa kuteuliwa kwake na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempatia heshima kubwa ya kuiongoza wilaya ya Chemba.

Adha aliwapongeza wakuu wengine wapya wa wilaya za Bahi Godwini Gondwe na Mpwapwa Sophia Kizigo waliohamishiwa mkoani Dodoma katika mabadiliko ya vituo vya wakuu wa wilaya yaliyofanyika hivi karibuni.

Hafla ya kumuapisha Mkuu wa wilaya ya Chemba na kuwakaribisha wakuu wa wilaya wapya ilifunguliwa na mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyemule ambayo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma, Viongozi  wa dini, Viongozi wa vyama vya siasa, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na Menejimenti ya Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment