Sunday, January 29, 2023

WANAOFANYA VITENDO VYA UKATILI WATAKIWA KUACHA MARA MOJA



Na Elizaberth Paulo,Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wanaume pamoja na wale wote wanaotenda vitendo vya kikatili kuacha mara moja kwani kundi kubwa linaloathirika na vitendo hivyo ni watoto na wanawake.

Aidha amesema mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo kuna vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Senyamule ametoa wito huo katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma (General Hospital) alipokua akizindua kituo jumuishi cha utoaji wa huduma kwa manusura wa vitendo vya Ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

"Mradi huu wa USAID AFYA YANGU umekuja wakati muafaka hapa Jijini na tunashukuru kwa sababu mkoa huu pia una changamoto ya vitendo vya kikatili,"amesema Senyamule.

Amesema kuwa manusura wa vitendo vya kikatili wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma kwa haraka na kwa taratibu kutokana na mtawanyiko wa maeneo ya huduma muhimu wanayohitaji ikiwemo huduma za afya, ustawi wa jamii na huduma za kisheria.

"Jengo hili la kutoa huduma jumuishi kwa manusura wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ni moja ya malengo ya mpango jumuishi wa utoaji huduma kwa walengwa iliyozinduliwa mwaka 2013 kwa lengo la kuhakikisha huduma inatolewa kwa manusura wa ukatili kwa haraka, uratibu mzuri, na kurahisisha mfumo wa rufaa kwa manusura kwa kupata huduma maalum kama msaada wa Kisheria,"amesema Senyamule.

Ameongeza kuwa hali hiyo imesababisha baadhi ya manusura kukosa huduma kwa wakati na kupata madhara yakiwemo maambukizi ya virusi vya Ukimwi, Ulemavu wa kudumu, mimba zisizotarajiwa na mimba za utotoni kutokana na vitendo vya ukatili alivyofanyiwa.

"Baadhi ya manusura kurubuniwa na kupoteza ushahidi ambao ungesaidia manusura kupata haki yake pindi shauri linapofikishwa katika vyombo vya Sheria, kutumia gharama kubwa katika kufikia maeneo ya kupatia huduma hivyo kusababisha matukio mengi ya ukatili kutokutolewa taarifa katika vyombo vya Sheria hali Iliyosababisha manusura kukosa huduma mbalimbali pamoja na haki za kisheria,"amesema Senyamule

Ameagiza wahudumu wa jengo ambalo wanatoa huduma kwa manusura kufanya kazi saa 24 kwani vitendo vya kikatili vinatokea muda wowote hivyo kuanzisha utaratibu wa kuwa katika hospitali hiyo muda wote na kuwaasa kutumia vifaa kwa umakini mkubwa na kwa weledi kwa manufaa ya kuchakata takwimu za manusura wanaopatiwa huduma katika jengo hilo lililozinduliwa ndani ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Kwa upande wake Chip Lyons Rais wa shirika la EGPAF ambao ni wadau waliofadhili ukarabati wa jengo hilo la utoaji wa huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili amesema mradi huo unatakribani miaka 13 tangu kuanzishwa kwake kutokana na ushirikiano mzuri na Viongozi wa Tanzania hata uongozi wa mkoa wa Dodoma.

Naye Anna Hoffman Naibu Mkurugenzi wa Shirika la afya la USAID amesema mradi huo Unatekelezwa katika mikoa Sita nchini ikiwemo mkoa wa Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tabora na Dodoma huku Ukilenga kufikia maeneo mengi hapa Tanzania.


No comments:

Post a Comment