Sunday, January 29, 2023

SHULE BORA KUINUA KIWANGO CHA UBORA WA ELIMU AWALI NA MSINGI

 


Na Wellu Mtaki, Dodoma

SERIKALI kupitia mradi wa Shule Bora wenye lengo la kuinua ubora wa Elimu ya awali na Msingi  utahakikisha unaongeza ufaulu wa masomo kwa wanafunzi kwa kuboresha ujifunzaji, Ufundishaji, kuimalisha Ujumuishi.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dk.Fatuma Mganga wakati akifungua mafunzo ya mpango wa Serikali wa SHULE BORA kwa waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Dk Mganga amesema kuwa moja ya malengo yaliyopo kwa sasa mkoani humo kwa mwaka 2023 ni kuongeza ufaulu kwa asili 95 ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba na asilimia 75 ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne wawe na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu.

"Suala la Elimu katika Mkoa wa Dodoma bado halijatangazwa vizuri na kuwataka waandishi wa habari wakatumie kalamu zao wakawe chachu katika kuielimisha jamii kuwa wanajukumu la kushiriki kikamilifu katika kuboresha elimu,"alisema Dk Mganga.

Amesema kuwa Mwaka huu peke yake zaidi ya wanafunzi 90,000 wanatarajiwa kuanza masomo ambapo hadi kufikia Januari 26  asilimia 89.7 ya wanafunzi wa darasa la awali wameripoti shule huku asilimia 94.2 kwa darasa la kwanza na asilimia 66.95 kidato cha kwanza wakiwa wameripoti shuleni.

Naye Mratibu wa mpango wa SHULE BORA Mkoa wa Dodoma Mtemi Zombwe amesema kuwa ili kufanikisha mchakato wa kuinua na kuboresha elimu ni vyema kila mmoja akatambua kuwa anajukumu la kushiriki katika mchakato huo.

Zombwe amesema kuwa katika ngazi ya kitaifa SHULE BORA itatoa pia msaada wa kiufundi kwa serikali ya Tanzania, pamoja na utekelezaji wa mradi wa pili wa LIPWA KWA MATOKEO yaani Education Program for Results Two.

Mradi wa Shule Bora ni Mpango wa Serikali ya  Tanzania, ikifadhiliwa na Serikali ya Uingereza kwa lengo la kuinua ubora wa elimu ya Awali na Msingi katika mikoa tisa hapa nchini kwa ushauri elekezi kutoka Cambridge Education ikishirikiana na mashirika ya ADD International, International Rescue Committee na Plan International.

No comments:

Post a Comment