CHONGOLO ATAKA VIJANA WAJENGEWE FIKRA ZA KIUCHUMI
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka viongozi wa vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika kuleta msukumo wa kuwajengea uwezo vijana kifikra na kiuchumi.
Chongolo meyasema hayo kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani wakati akifungua kikao kazi cha makatibu wakuu wa vyama rafiki wanaounda kamati ya usimamizi wa shule hiyo.
Chongolo amesema kuwa Ukombozi wa nyuma ulikuwa ni wa kujikomboa kutoka kwa wakoloni lakini kujikomboa kwa sasa ni kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kifikra.
"Makatibu Wakuu kutoka nchi sita marafiki wanapaswa kudumisha uzalendo ulioasisiwa na viongozi waliotangulia ambao waliweka misingi ya ushirikiano,"alisema Chongolo.
Aidha amesema kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan anawakaribisha nchini huku akiwawakikishia usalama wao kwa muda wote watakaokuwa hapa nchini hadi watakaporudi makwao.
"Mwaka jana tulipokutana tulijadili mambo mengi kwa kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao sasa leo tumekutana ili tuweze kuchakata kwa kina yale yote tuliyojadili,"amesema Chongolo.
Naye Katibu Itikadi na Uenezi CCM Sophia Mjema amesema kuwa kila kitakachokifanyiwa maamuzi kitajengwa katika sura ya umoja kama ulivyojengwa katika historia ya nchi hizo rafiki.
Vyama hivyo vilivyoshiriki ni CCM Tanzania, ZANU PF Zimbabwe, FRELIMO Msumbiji, MPLA Angola, SWAPO Namibia na ANC Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment