Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Afya cha Mkoani kinakabiliwa na changamoto ya
ukosefu wa Jenereta ili kukabiliana na tatizo la ukatikaji umeme kwenye chumba
cha akinamama wanapojifungulia hivyo kuwaomba wadau mbalimbali.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mganga mkuu wa Halmashauri ya
Mji wa Kibaha Happiness Ndosi wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali kwa
watoto waliozaliwa na watakaozaliwa kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la
Abubaker Darwesh International Charitable Foundation (ADICF) la Jijini Dar es
Salaam.
Dk Ndosi alisema kuwa kukatika kwa umeme kwenye kituo hicho
ni changamoto kubwa hasa nyakati za usiku na wakati mama wajawazito wanapokuwa wanajifungua
hali ambayo inahatarisha maisha ya akinamama hao.
“Kutokana na hali hiyo tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze
kutusaidia kupata jenereta kwa ajili ya kusaidia mara umeme unapokatika katika
chumba cha uzalishaji mama wajawazito ili kunusuru maisha yao,” alisema Dk
Ndosi.
Aidha alisema mbali ya changamoto hiyo pia wanakabiliwa na
changamoto nyingine ikiwa ni pamoja na ukosefu wa chumba cha upasuaji, Ultra
Sound na X-Ray, gari la wagonjwa kwani lililopo ni chakavu, magodoro na vitanda
hasa ikizingatiwa kuwa kituo hicho kiko mbioni kuwa Hospitali ya Wilaya.
Kwa upande wake mwanzilishi na meneja mradi wa shirika hilo
Bilal Abubekar alisema kuwa shirika lake limeamua kutoa misaada hiyo kwa lengo
la kuisaidia jamii hasa kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano ili
kuisaidia serikali kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma
bora.
Abubaker alisema kuwa shirika lao limekuwa likisaidia makundi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajane yatima na watu wenye mahitaji, pia
kusaidia elimu watu wenye ulemavu.
Naye moja ya wagonjwa waliopata msaada huo Mariamu Ally alishukuru
shirika hilo na kusema kuwa wameonyesha moyo wa upendo na kuwataka waendelee
kusaidia hospitali hiyo ili iweze kukabiliana na changamoto zilizopo kwa
wagonjwa.
Alisema kuwa moja ya changamoto iliyopo kwenye wodi hiyo ni
kuchanganywa kati ya akinamama waliojifungua na wale wanaosubiri kujifungua na
kutaka watu hao kutenganishwa ili kila moja wawe na sehemu yao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la Mwenyekiti wa Mtaa wa Muheza kata ya Maili Moja wilayani
Kibaha mkoani Pwani Maulid Kipilili limechukua sura mpya baada ya wananchi wa
mtaa huo kumkataa mwenyekiti huyo kwenye mkutano wa wananchi uliofanyika mtaani
hapo.
Wananchi hao walimkataa mwenyekiti wao wakati wa mkutano
ulioitishwa na diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi ili kujadilia
suala la malalamiko ya wananchi wa mtaa huo baada ya kuifunga ofisi ya mtaa
hadi pale watakapofikia muafaka juu ya mwenyekiti wao.
Mkutano huo ambao ulifanyika mtaani hapo chini ya diwani huyo
wa kata na ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Thadeo Mtae wananchi hao walilalamika
kuwa mwenyekiti wao tangu achaguliwe kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni
mwa mwaka 2015 hajaitisha mkutano wa wananchi.
Kabla ya kufikia hatua ya kumkataa mwenyekiti wao wananchi
hao walitoa malalamiko yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulalamika kuwa mwenyekiti
wao haitishi vikao vya wananchi, hasomi mapato na matumizi, kutofungua ofisi
hivyo kuwapa shida wananchi wanapokwenda kupata huduma za kiofisi.
Akizungumza juu ya mwenyekiti wao kushindwa kuwajibika mwananchi
wa mtaa huo Kitai Mganga alisema kuwa ni pamoja na tuhuma nyingine ni kushindwa
kusimamia mali za mtaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kumega na kuuziana
eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Msingi lakini hakuna hatua
zozote ambazo amezichukuwa.
“Mtaa wetu una changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu
wa maji, umeme, Shule ya Msingi, bararabara na zahanati lakini kutokana na
mwenyekiti wetu kutowajibika tumeshindwa kufanya lolote hata kuweka mikakati ya
maenedeleo hakuna,” alisema Mganga.
Naye Paulo Chacha alisema kuwa mwenyekiti lazima awe na
wajumbe wa mtaa lakini cha kushangaza wajumbe hawapo hivyo mwenyekiti anafanya
kazi peke yake jambo ambalo haliwezi kuleta mafanikio.
Chacha alisema kuwa kamati ya mtaa ni sawa na baraza la
mawaziri sasa haiwezekani Rais kuongoza nchi bila ya kuwa na Mawaziri kwani
maendeleo hayawezi kupatikana.
Kwa upande wake Maulid Kipilili alisema kuwa kwa upande wa
mikutano alishindwa kufanya kutokana na sababu maalumu ikiwa ni pamoja na
shughuli za kitaifa.
Kipilili alisema kuwa aliitisha mikutano mitatu ya dharura na
miwili ya kikatiba na kuwashangaa wananchi hao kumsingizia kuwa hajafanya
kabisa mikutano na mmoja wa Mei 15 ulishindwa kufanyika kutokana na akidi
kushindwa kuenea.
“Kuhusu wajumbe wa serikali ya mtaa hawajafika kwa sababu
mbalimbali lakini wapo na sina mgogoro na wajumbe wangu na tunafanya kazi
vizuri na baadhi ya kamati zipo na zinafanya kazi kama ya maji na shule zipo na
aliyeuziwa eneo la shule kama kuna mtu anaushahidi alete ili tuchukue hatua za
kisheria,” alisema Kipilili.
Akielezea juu ya changamoto hiyo ya wananchi kumkataa
mwenyekiti wao diwani wa kata hiyo Ramadhan Lutambi alisema kuwa kama hawamtaki
wanapaswa kufuata taratibu kwani hatua ya kwanza ni hiyo.
Lutambi alisema kuwa kutokana na hali hiyo itabidi uitishwe
mkutano wa dharura wa kata kujadili suala hilo na wao ndiyo watakaoamua hatma
ya mweneyekiti wao.
Kufuatia kukataliwa na wananchi ofisa mtendaji wa kata ya
Maili Moja Thadeo Mtae alisema kuwa hoja zilizotolewa ni 15 ambapo zimejibiwa
na mwenyekiti huyo ambapo baadhi wamekataa majibu yake na nyingine wamekubali
majibu.
Mtae alisema kuwa atapeleka sehemu husika kwa ajili ya majibu
na hatua zaidi kwani yeye hatoweza kutoa majibu hivyo wasubiri majibu ambapo
kutaitishwa mkutano mwingine.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakazi kwneye eneo la Sagulasagula maarufu kama
Loliondo Mtaa wa Machinjioni kata ya Tangini wilayani Kibaha mkoani Pwani
wanaodaiwa kuvamia eneo lililotengwa kwa ajili ya soko wameiomba Halmashauri ya
Mji kuwalipa fidia na maeneo ya kuishi baada ya kupewa siku 14 kuhama kwenye
eneo hilo.
Wakizungumza mara baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya
Wilaya kupitia na kuangalia eneo hilo na kutoa maagizo kwa wakazi hao kubomoa
nyumba zipatazo 55 zilizojengwa kwenye eneo hilo walisema kuwa kwa kuwa ni
mpango wa maendeleo basi nao waangaliwe kwani wamekaa hapo kwa muda mrefu.
Said Tekelo alisema kuwa baadhi ya watu wako hapo tangu mwaka
1970 na mwaka 2003 Rais Benjamin Mkapa wakati ule alifuta hati ya eneo hilo
toka eneo la Viwanda na kutaka lirejeshwe kwenye mtaa kwa ajili ya matumizi
mengine.
“Baada ya kurejeshwa kwenye mtaa baadhi ya watu walipimiwa
maeneo yao baada ya kupigwa picha na kamahaitoshi hata alipokuja waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa miezi mitatu sasa sita Halmashauri
ikae na wakazi hao ili kujadili namna nzuri ya kufanya,” alisema Tekelo.
Alisema kuwa licha ya maagizo hayo walikwenda Mahakamani
kwenda kulalamika walipotakiwa kuondoka na kesi iliendeshwa na wao kushindwa na
Mahakama ili amuru Halmashauri ikae nao lakini hakuna kilichofanyika hadi
mwishoni mwa wiki walipotakiwa kuvunja wenyewe na endapo hawatafanya hivyo
Halmashauri itabomoa nyumba hizo.
“Tumeambiwa tubomoe wenywe na kuanzia leo Tanesco na Dawasco
wameshapewa maagizo ya kuondoa miundombinu yao ilkiwa ni maandalizi ya kubomoa
sisi tunaomba Halmashauri itufikirie kwa kutulipa fidia pamoja na maeneo kwa
ajili ya kuishi kwani wenzetu jirani ambao tuko kwenye mgogoro mmoja wamelipwa
na kupewa viwanja,” alisema Tekelo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Tangini Theodori Joseph
alisema kuwa suala hilo ni la muda mrefu ambapo baraza la Madiwani miaka ya
nyuma waliwatambua wakazi hao kutaka walipwe fidia na walikuwa wakishirikiana
nao katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchukua kodi za majengo.
Joseph alisema kuwa kuna haja ya Halmashauri kuwafikiria
wakazi hao kwani wengine wako hapo miaka 40 iliyopita na wameendeleza ardhi kwa
kipindi chote hicho lakini jirani zao ambao wametengwa na barabara wao wamepewa fidia na watapewa viwanja.
Ofisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Inocent
Byarugaba alisema kuwa eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya soko na liko kwenye
Ramani ya Mji na wakazi hao walilivamia
eneo hilo na wanapaswa kuliachia.
Byarugaba alisema kuwa tayari eneo hilo liko kwenye
maandalizi ya ujenzi wa soko unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa
kwani tayari ramani imeshatoka ambapo soko linalotumika kwa sasa liko kwenye
hifadhi ya barabara na litabomolewa muda wowote na Tanroads.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Lucy Kimoi alisema kuwa
wakazi hao wanapaswa kuondoka na kwa sasa wanaandaa notisi kwa ajili ya
kuwataka waliachie eneo hilo kwani wako hapo kinyume cha Sheria.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani imetenga kiasi cha
zaidi ya shilingi milioni 990 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa kwenye eneo
la mnada wa kila wiki maarufu kama
Sagulasagula au Loliondo kwa ajili ya wakazi wa mji huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha
ofisa habari wa Halmashauri hiyo Inocent Byarugaba alisema kuwa soko hilo
litachukua wafanyabiashara wapatao 286 ambao walikuwa kwenye soko la zamani la
Maili Moja ambalo linatarajiwa kubomolewa.
Byarugaba alisema kuwa lengo la kujenga soko hilo kubwa na la
kisasa ni kutaka kuwarahisishia wananchi kupata huduma bora badala ya
kukimbilia kwenye maosko makubwa kama vile la Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
“Tutajenga kwa kushirikiana na wananchi kwa mtindo wa jenga,
endesha na rudisha (BOT) ambapo
watajenga kwa mkataba maalumu ambao utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili,”
alisema Byarugaba.
Alisema kuwa ujenzi huo wa soko hilo utahusisha maduka ya
jumla na rejareja, sehemu ya kuuzia mazao ya nafaka, samaki, mabucha ya nyama
10, mbogamboga, sehemu ya kuchinjia kuku, matunda na sehemu ya kupaki magari.
“Lengo ni kuwa na huduma bora ya soko kwani lililopo lilikuwa
ni dogo na halikuwa na huduma nyingi kutokana na ufinyu wake na mabanda yake
yalijengwa kwa muda kutokana na kuwa kwenye hifadhi ya barabara ambapo wenywe
wanalitaka eneo lao kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo,” alisema Byarugaba.
Aidha alisema kuwa ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kuanza
wakati wowote kwani tayari ramani imeshachorwa kinachosubiriwa ni taratibu
chache zilizosalia ili kuanza kazi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MADEREVA wa mabasi ya abiria yanayopita mkoani Pwani
wametakiwa kuacha tabia ya kutumia vilevi ikiwemo pombe ili kuepusha ajali ambazo
zimekuwa zikileta madhara na uharibifu wa mali ulemavu na kupoteza maisha ya
abiria wanaowasafirisha.
Hayo yamesemwa na mwalimu wa kufundisha matumizi ya vifaa vya
kupima ulevi wa Jeshi la Polisi mkoani humo Aisha Sudi na kusema kuwa moja ya
vyanzo vikuu vya ajali vinatokana na ulevi hususani ule wa pombe.
Sudi amesema kuwa dereva wa basi hapaswi kabisa kutumia pombe
pale anapokuwa akiendesha gari licha ya kuwa ulevi chini asilimia 80 ni wa
kawaida ila unapozidi zaidi ya hapo ni hatari kwa uendeshaji wa gari.
Amesema kuwa wanapowapima na kuwabaini wana vilevi
hawaruhusiwi kuendesha basi na kutakiwa kubadilisha dereva ili kuendelea na
safari na hali hiyo imesababisha kupungua kwa ajali katika mkoa huo.
Aidha amesema kuwa hufikia kuyakagua mabasi hayo baada ya
kupata taarifa toka kwa abiria ambao wanaangalia mwenendo wa dereva au
wanapomtilia shaka dereva wa basi na anapobainika kutumia kilevi anapelekwa
mahakamani kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama
Barabarani mkoani humo Abdi Issango amesema kuwa vifaa hivyo vinatumika kwenye
maeneo mbalimbali kwenye barabara za kwenda mikoa jirani ya Tanga, Morogoro na
Lindi.
Issango ametaja maeneo ambapo kuna askari wanaotumia hivyo
vifaa kuwa ni pamoja na Maili Moja, Mlandizi, Vigwaza, Chalinze, Mdaula, Wami
Mbwewe, Mapinga, Kiwangwa, Vikindu, MKuranga, Kimazinchana na Kibiti.
Amesema kuwa kutokana na Jeshi la Polisi kuweka mikakati
mbalimbali ya kuzuia ajali katika kipindi cha Januari hadi Aprili hakuna ajali
kubwa ya basi iliyosababisha vifo kwani nyingi ni zile ndogondogo ambazo hazina
madhara makubwa.
Amebainisha kuwa ajali zinazoleta madhara kwa sasa ni za
pikipiki kutokana na madereva wengi wa bodaboda kutozingatia sheria za usalama
barabarani ambapo wengi hawana leseni kwani biashara hiyo ilianza bila ya
utaratibu ambapo kwa sasa wanaendelea kuwapatia elimu ili waendeshe vyombo
hivyo kwa kuzingatia sheria.
Mwisho.