Sunday, April 21, 2024

GOODWILL NA SAPPHIRE GLASS ZATOA MISAADA KWA WAHANGA WA MAFURIKO RUFIJI



KAMPUNI ya utengenezaji Marumaru ya GoodWill na ya Vioo ya Sapphire Glass za Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani zimetoa misaada mbalimbali kwa wahanga wa mafuriko Wilayani Rufiji.

Akikabidhi misaada hiyo ofisa rasilimali watu wa GoodWill Jerry Marandu kwa mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta amesema wameungana ili kusaidia wahanga hao wa mafuriko.

Marandu ambaye pia aliwakilisha kampuni ya Sapphire Glass amesema kuwa misaada hiyo ni unga wa sembe mifuko 70, mchele mifuko 10 na sabuni mifuko 20 ambavyo wameona vitasaidia sehemu ya mahitaji kwa walengwa hao wa mafuriko.

Naye Katibu Tawala Rashid Mchatta amezishukuru kampuni hizo kwa kujitolea kusaidia jamii kwani ni moja ya jukumu lao hivyo kuiunga mkono serikali kusaidia wananchi wake.

Mchatta amewaomba wadau wengine nao kuunga mkono kwa kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ili kuwapunguzia changamoto wananchi waliokumbwa na mafuriko kwenye Wilaya za Rufiji na Kibiti.





Saturday, April 20, 2024

SHIRIKA LA (THPS) LATOA MSAADA KWA WAHANGA WA MAFURIKO RUFIJI NA KIBITI

  







SHIRIKA la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limetoa msaada wa vifaa vya shule na vyakula kwa wahanga wa mafuriko katika Wilaya za Rufiji na Kibiti Mkoani Pwani.
Misaada hiyo ilikabidhiwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Bodi Profesa Mohamed Janabi ambaye amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa (THPS) Dk. Redempta Mbatia, viongozi kutoka Serikali za Mkoa wa Pwani na Wilaya za Rufiji na Kibiti, wahudumu wa afya, maofisa wa THPS na wananchi wenye mapenzi mema.

Prof Janabi amesema msaada huo wenye thamani ya Shilingi milioni 18.8  ni pamoja na vifaa vya shule  zikiweno sare za shule, mabegi, madaftari na kalamu vyenye thamani ya shilingi milioni 7.8 huku kwa upande wa vyakula ni pamoja na unga wa mahindi kilo 1,500, maharage kilo 750 na mafuta ya kupikia dazeni 29.5 vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 10.9.

Amesema kuwa mahitaji hayo yanatarajiwa kutoa ahueni kwa waathirika wa mafuriko wakati wakijpanga kurejea kwenye shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.

"THPS na wao kama moja wapo ya wadau wakubwa wa afya wanaofanya kazi mkoani Pwani tumeungana na Serikali katika jitihada za kusaidia watu waliokumbwa na mafuriko,"amesema Prof Janabi.

Aidha amesema kuwa wanatumai msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha wanayoipata wakazi wa Wilaya za Rufiji na Kibiti waliokumbwa na mafuriko.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe.  Abubakar Kunenge alitoa shukrani zake kwa THPS kwa msaada huo na kusema kuwa anatarajia kuendelea kushirikiana na Shirika hilo.

Kunenge amesema kuwa msaada huo utasaidia kuleta matumaini kwa watu waliopoteza mali na makazi kutokana na mafuriko hayo.

THPS ni Shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 2011 na kupitia uimarishaji wa mifumo ya afya na jami linalenga katika kushughulikia changamoto mbalimbali za afya ya umma, ikiwa ni pamoja na VVU na UKIMWI, kifua kikuu, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, huduma za afya ya uzazi, watoto wachanga, watoto nĂ£ vijana, maabara na mifumo ya taarifa za usimamizi wa afva, UVIKO- 19 na tathmini za afya ya umma.








Friday, April 19, 2024

KUNDI LA KIBAHA HURU FIKRA HURU LATOA MADAWATI 30

KUNDI la Whatsapp la Kibaha Huru Fikra Huru limetoa msaada wa madawati 30yenye thamani ya shilingi milioni tatu ili kusaidia wanafunzi ambao wanakabilia na upungufu wa madawati kwenye Shule za Msingi za Halmashauri ya Mji Kibaha.

Mwenyekiti wa Kundi hilo la Kijamii Mchungaji Paschal Mnemwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mara baada ya kukabidhi madawati hayo amesema wameguswa na changamoto ya wanafunzi hao kukaa chini.

Mch Mnemwa amesema kuwa wameamua kuchangia madawati hayo ili kuisaidia serikali ili kukabiliana na changamoto hiyo ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.

"Nawashukuru wana kikundi na watu mbalimbali kwa kutoa fedha na huu siyo mwisho kwani huo ni mwanzo wa kusaidia kumfuta vumbi mtoto wa Kibaha ili kumfanya mtoto awe na moyo wa kusoma na wadau mbalimbali wajitoe kusaidia tujenge tabia kusaidia maendeleo,"amesema Mnemwa. 

Amesema jamii isitegemee misaada toka nje bali ianze kuchanga yenyewe ili kusaidiana wenyewe kwa wenyewe badala ya kusubiri kusaidia kutoka nje ya nchi wafadhili wa kwanza iwe jamii yenyewe ili kuleta maendeleo.

"Mifumo ya mitandao ya kijamii ilitengenezwa ili kuiweka jamii pamoja kusaidiana na wasiitumie vibaya kwani endapo itatumika vibaya itaharibu maadili ya jamii ikitumika vizuri inaweza kuleta maendeleo,"amesema Mnemwa.

Akipokea madawati hayo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anawashukuru na kuwapongeza kundi hilo kwa kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujitolea madawati hayo.

Ndomba amesema kuwa madawati hayo yatasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati kwenye shule mbalimbali za Mji wa Kibaha na kuwataka wadau wengine kuchangia kama walivyofanya kundi hilo.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Taaluma wa Halmashauri ya Mji Kibaha Adinani Livamba amesema kuwa wana upungufu wa madawati zaidi ya 3,000 ambapo madawati ni hitaji kubwa kwani wanafunzi wanafunzi wanaongezeka pia yanaharibika hivyo changamoto hiyo haiwezi kwisha kabisa.

Livamba amesema kuwa wanachukua hatua mbalimbali kukabili changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa madawati 1,321 na wanafanya na matengenezo na madawati hayo yatasaidia wanafunzi 90 wa darasa la kwanza, la pili na la tatu ambao ndiyo watanufaika.

Naye msemaji wa kundi hilo Hamis Mponji amesema kuwa fedha zimechangwa na watu wa Kibaha na nje ya Kibaha ambapo kulikuwa hakuna kiwango maalum cha kuchanga ni kile ambacho mtu kaguswa kukitoa.

Moja ya viongozi wa kundi hilo Hamad Kibwelele amesema kuwa wakati wanaanzisha kundi wakaona lisiwe na maongezi tu bali wafanye kitu cha maendeleo kwenye jamii na kukubaliana kuchangia madawati huku wakiangalia nini cha kufanya kwa baadaye ili kuleta maendeleo Kibaha.

Tuesday, April 16, 2024

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAONGEZA MELI ZA UVUVI BAHARI KUU

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu  (Deep Sea Fishing Authority-DSFA) imefanya maboresho katika kanuni za Sheria Uvuvi wa Bahari Kuu  na kupandisha utoaji wa vibali vya uvuvi katika Bahari Kuu kutoka  meli tisa mwaka 1988 hadi meli 61 mwaka 2023/24 kwa ajili ya kufanya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) upande wa Tanzania.

Hayo yamesemwa Leo Tarehe 16 Aprili 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Muungano kuelekea maadhimisho ya miaka 60.

Ameeleza kuwa DSFA imeingia mkataba na Kampuni ya Albacora ya nchini Hispania kwa ajili ya ujenzi wa  kiwanda cha kuchakata samaki katika Mkoa wa Tanga na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 20 za samaki kwa siku, kuhifadhi tani 2,400 za samaki na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 100.

Pia amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukitumia Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Machui – Tanga kupata vifaranga vya samaki na viumbe maji wengine wakiwemo jongoo bahari kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa buluu.

Aidha, zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanakadiriwa kupata kipato chao cha kila siku kutokana na shughuli za Uvuvi, zikiwemo kuunda na kutengeneza boti, kushona nyavu, biashara ya samaki na mazao yake pamoja na Baba na Mama lishe. 

Ikumbukwe kuwa sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta tatu za Kilimo ambazo zinaajiri wananchi wengi na imeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji wapatao 35,986.

SERIKALI YATOA BILIONI 696.7 KUPUNGUZA UMASKINI

SERIKALI imetoa shilingi bilioni 696.7 kwa ajili ya kupunguza na kuondoa umaskini kwa kaya milioni 1.3 kwenye vijiji  na mitaa.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano.

Simbachawene amesema kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato.

Amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na serikali  mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii.

"Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF awamu ya I awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya,”amesema Simbachawene.

Simbachawene amesema awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi 2013 katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar.

Amefafanua kuwa  jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).

Amesema katika miaka 60 ya Muungano, serikali inayoongozwa na Rais,  Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.

Aidha amesema kuwa TAKUKURU kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa.

Pia amesema Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na ni “Jeshi kubwa” ambalo tumeshuhudia likitoa mchango chanya katika matukio mbalimbali ya kijamii na kitaifa.

WANAOTUKANA VIONGOZI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni amesema kuwa  wanaotumia mitandao kuwatukana viongozi wa nchi  watakumbana na mkono wa sheria popote walipo.

Masauni ametoa kauli hiyo Aprili 15/2024  katika kumbi wa habari Maelezo Jijini  Dodoma alipokuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua watu wanaomtukana Rais Samia katika mitandao.

Amesema kuwa hawatakuwa na msamaha  kwa mtu yoyote atakayevunja sheria ya kutukana viongozi na atatafutwa popote mpaka apatikane.

‘’Mimi niseme tu Serikali haina msalie mtume kwa mtu yeyote anayevunja sheria kwa kutukana viongozi katika mitandao na ina mkono mrefu wanaofanya hivyo watatafutwa popote walipo mkono wa sheria utawakamata,’’amesema Masauni.

Aidha Masauni ambaye alikuwa akielezea mafanikio ya miaka 60 ya Muungano amesema tangu enzi za waasisi wa Muungano Mwalimu Nyerere na Amani Karume walijenga Taifa lenye maadili hivyo ni budi kuendeleza yale waliyoacha waasisi wetu.

Sambamba na hayo ametoa wito kwa wananchi kuwa Serikali haitamfumbia macho mtu au kikundi cha watu wanaotukana viongozi kupitia mitandao  kwa kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

‘’Msifikirie haya mambo yanayoenendelea mitandaoni na kutukana watu hawachukuliwi hatua utajikuta na wewe unafuata mkumbo usiige kwani hakuna atakayeachwa salama,"amesema Masauni.

Waziri huyo amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwani Serikali ya Rais Samia haipendi kusumbua watu inataka watu waishi kwa amani na kila mmoja atii sheria bila shuruti.

‘’Dhamira ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapendi kuona watoto wake wanapata shida hivyo vyombo vya usalama vipo kazini’’, amesema Masauni.

Pia amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano sekta ya usalama wa nchi  iko vizuri na mafanikio ni mengi ikiwemo kuwa na majeshi ya polisi imara.

Sunday, April 14, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA PWANI YATOA SHUKRANI KWA CHUO CHA VETA MKOA WA PWANI KUWAPATIA USAFIRI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA 102 KUZALIWA KWA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA DODOMA




Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani ndugu Omary Abdul Punzi kwa niaba ya uongozi ameshukuru chuo cha Veta Pwani kupitia Mkuu wa chuo hicho Madam Crala Kibodya kuwezesha safari hiyo kwa kutoa usafiri wa Coaster.

Ndugu Omary Punzi amesema huo ni uzalendo mkubwa kawa wadau nchini wasisite kusaidia katika shughuli nyingine.

Maadhimisho hayo yaliyofana yaliyohudhiliwa na Wananchi wengi wanafunzi na makundi mengine Mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Dkt Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.