Saturday, June 13, 2026

*SERIKALI YADHAMIRIA KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO NCHINI*

▪️Taarifa ya mapendekezo ya kuwaendeleza Wachimbaji wadogo yawasilishwa

▪️Prof Mkumbo aeleza umuhimu wa sekta ya madini kufikia Dira 2050

Lengo ni Kuongeza Ajira, Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi

▪️Mfuko wa Dhamana  kutatua changamoto ya mitaji kwa wachimbaji

▪️Serikali yaanzisha mfuko wa Madini kwa ajili ya Utafiti wa Madini

📍 Dar Es Salaam

Serikali imesisitiza kufanyia kazi kwa haraka Mapendekezo yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu iliyoundwa Kuishauri Wizara ya Madini kuhusu namna ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo Kiuchumi na kueleza kuwa, utatuzi wa changamoto za Mitaji, Teknolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi za Kijiolojia kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini ni hatua muhimu ya kuongeza ajira kwa watanzania, kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa Taifa kuelekea Dira 2050.

Hayo yamebainishwa Juni 13, 2026 jijini Dar Es Salaam  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya Kupokea Mapendekezo ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo Nchini na kusisitiza kwamba, maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mipango ya maendeleo inajibu changamoto tatu kuu za taifa ambazo ni kuongeza mitaji kwa wananchi, kuzalisha ajira na kupunguza umaskini.

Amesema kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji na teknolojia, kunafungua fursa za kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi na kuongeza kuwa hiyo ndiyo njia mojawapo ya kupambana na umaskini.

‘’Kazi kubwa ya Waziri ni kutoa mwelekeo wa kisera wa taasisi au wizara anayoiongoza. Kwa muda niliokaa kwenye Wizara yangu, Mhe. Mavunde amekua akijua kipaumbele anachokitaka na jinsi ya kukipata,’’amesisitiza Prof. Mkumbo.

Ameongeza kwamba, hali ya umaskini nchini  bado ipo kwa kiwango cha juu na kutolea mfano wa Mkoa wa Geita ambao unaoongoza kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu nchini ambapo  hali ya umaskini inafikia asilimia 38 na kusisitiza kwamba, wachimbaji wadogo wanapowezeshwa wanasaida kutatua changamoto kama hizo na kuongeza kuwa, Sekta ya Madini imewekwa kama moja ya sekta muhimu za kimageuzi  inayotarajiwa kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na ajira ambapo awali haikuwa ikibeba watu wengi.

Naye, Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza katika halfa hiyo, amesema Serikali iliamua kuunda kamati hiyo kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na wachimbaji wadogo katika Sekta ya Madini, licha ya kukabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia na upatikanaji wa huduma za kifedha , hivi sasa wanachangia asilimia 40 ya makusnyo ya maduhuli ya Serikali.

Ameongeza kwamba, kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta ya Madini ndani ya miaka ya hivi karibuni yanaonyesha umuhimu wa kuwawezesha zaidi wachimbaji wadogo ili waongeze mchango wao katika uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Mwaka wa Fedha  2015/16 Sekta ya Madini katika mwaka mmoja iliingiza shilingi bilioni 161 pekee katika Mfuko Mkuu wa Serikali. 

Hata hivyo, kufuatia mageuzi mbalimbali yaliyofanyika ikiwemo mabadiliko ya sheria, kuanzishwa kwa masoko ya madini na udhibiti wa biashara haramu ya madini, makusanyo yameongezeka kwa kiwango kikubwa kufikia Shilingi trilioni 1.107 mwaka 204/25 na mpaka kufikia  tarehe 13, Juni, tayari Serikali imekusanya shilingi trilioni 1.3.

Amesisitiza kuwa jukumu la Serikali yoyote duniani ni kuwawezesha wananchi wake kufanya shughuli za uzalishaji kwa tija zaidi sababu ambayo ilipelekea  Serikali kuweka mkakati maalum wa kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kukua na kuwa wachimbaji wa kati na baadaye wakubwa.

Kuhusu changamoto ya mitaji, Waziri Mavunde  amesema Serikali imeanza utekelezaji wa Kampuni ya dhamana ya mikopo (Credit Guarantee Corporation) itakayosaidia  wachimbaji kupata mikopo kutoka taasisi za fedha mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo  Dkt. Victor Tesha  amesema suluhu ya changamoto hizo ni kujenga mfumo jumuishi wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia upatikanaji wa mitaji, teknolojia za kisasa, taarifa za kijiolojia na uratibu wa taasisi zinazohusika na sekta hiyo huku akipendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Madini Tanzania utakaowezesha miradi yenye sifa kupata fedha za kuendeleza uzalishaji, kununua mitambo na kuboresha shughuli za uchimbaji, na kuongeza kwamba, mfuko huo utasaidia kugharamia tafiti na taarifa za kijiolojia kwa wachimbaji.

Ameongeza kuwa, baada ya mfuko huo kukua na kuimarika, hatua itakayofuata itakuwa ni kuanzisha Benki ya Wachimbaji itakayotoa huduma maalumu za kifedha kwa sekta ya madini kwa masharti yanayoendana na mazingira ya wachimbaji.

‘’Kamati pia imependekeza mikopo ielekezwe zaidi katika ununuzi wa mitambo na teknolojia badala ya fedha taslimu pekee, ili kuongeza tija, uzalishaji na usalama katika shughuli za uchimbaji,’’ amesema Tesha.


 Naye, rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Wadogo John Bina, ameipongeza Serikali kwa ripoti hiyo na kueleza imetokana  na Serikali kusikiliza na kuyafanyia kazi maoni na changamoto za wachimbaji wadogo, pamoja na kuipongeza kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yanayotokana na shughuli za madini kwa ajili ya utafiti.

No comments:

Post a Comment