Tuesday, June 9, 2026

POLISI PWANI KUFANYA UCHUNGUZI KISAYANSI KUCHUNGUZA MADAI MZAZI KUBADILISHIWA MTOTO

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linafanya uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi ili kubaini ukweli juu ya lalamiko la mwanamke aitwaye Filomena Mataris (36) Mkazi wa Gongo la Mboto Dar es Salaam kudai kubadilishiwa mtoto baada ya kujifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.

Uchunguzi huo unafanyika baada ya mlalamikaji kudai kuambiwa mtoto wake aliyejifungua amefariki na kuzikwa pasipo yeye na mume wake kushiriki mazishi ya mtoto wake ambapo alizikwa na ndugu zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase alisema kuwa Juni 5 mwaka huu Filomena Mataris akiwa na mume wake Caros Kapata walifika kituo cha Polisi Bagamoyo wakilalamika kubadilishiwa mtoto kwenye Hospitali ya Bagamoyo. 

Morcase alisema kuwa walipofika polisi walieleza kuwa Aprili 14 mwaka huu Filomena Mataris alihamia Kerege Wilayani Bagamoyo kwa mtoto wa dada yake aitwaye Avetha Mabadiliko kwa ajili ya uangalizi wa karibu akitokea Gongo la Mboto Dar es Salaam.

"Mnamo Mei 17 mwaka huu majira ya saa 3:000 asubuhi Mataris alipata uchungu wa kujifungua hivyo aliongozana na ndugu yake huyo Mabadiliko kwenda Hospitali ya Kerege kwa ajili ya kujifungua,"alisema Morcase.

Alisema kuwa baada ya kufika hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo daktari alibaini Mataris ana dalili ya uzazi pingamizi hivyo alielekeza apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

"Iipofika Mei 18 mwaka huu majira ya saa 8:00 usiku Mataris alihamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ambapo saa 8:30 usiku alijifungua mtoto wa kiume kwa njia ya upasuaji na alieleza kuwa alimuona mtoto wake na kumbeba akiwa mzima wa afya,"alisema Morcase.

Aidha alisema Mataris alisema kuwa baada ya kupewa huduma na kwenda wodini alioneshwa picha za mtoto kwenye simu ya daktari na kuambiwa ndiye mtoto wake na ameshafariki. 

"Mtoto aliyeonyeshwa kwenye picha alikuwa na changamoto kama vile kichwa kubonyea na kuwa na uvimbe kifuani tofauti na mtoto wake aliyembeba baada ya kujifungua,"alisema Morcase.

Aliongeza kuwa baada ya kuonyeshwa picha hizo aliambiwa na daktari kuwa mwili umekabidhiwa kwa ndugu zake ambao ni Mabadiliko na shangazi
yake aitwaye Adora Mathias kwa ajili ya mazishi. 

"Mtoto huyo alizikwa bila uwepo wa Mataris ambaye ni mama wa mtoto wala baba wa
mtoto hakufahamishwa kuhusu mazishi hayo na mara baada ya kupata taarifa hiyo kutoka kwa familia hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilifungua jalada la uchunguzi lenye
namba BAG/PE/33/2026,"alisema Morcase.

Aliongeza kuwa Polisi walianza ufuatiliaji ulianza ambapo walimhoji Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo Dk. Mariam Ngwele aliyeeleza kuwa baada ya kumpokea Mataris.

Alisema kuwa Dk Ngwele alieleza kuwa Mataris  alijifungua kwa njia ya upasuaji lakini mtoto hakuwa wa kawaida kwani alikuwa na kichwa kilichobonyea na uvimbe sehemu ya kifuani na changamoto ya upumuaji hivyo alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Kamanda Morcase alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea na uchunguzi zaidi wa kitaalamu
na kisayansi ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment