Na Albert Kawogo
TANGU Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ateuliwe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Global Partnership for Education mwezi Septemba 2021, taasisi hiyo imeendelea kuimarisha juhudi za kuboresha elimu katika nchi zinazoendelea duniani.
Dkt. Kikwete akiwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kushika nafasi hiyo muhimu katika historia ya shirika hilo,chini ya uongozi wake, GPE imeongeza juhudi za kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata elimu bora, hususan wale wanaotoka katika mazingira magumu, maeneo yenye migogoro, wakimbizi na watoto wenye ulemavu.
Taasisi hiyo imeendelea kushirikiana na serikali mbalimbali duniani kuboresha mifumo ya elimu na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo ambapo ufanisi mkubwa umeonekana.
Moja ya mafanikio makubwa yaliyoshuhudiwa ni kuongezeka kwa ufadhili wa miradi ya elimu katika nchi wanachama. Katika kipindi cha mkakati wa GPE 2025, mamia ya mamilioni ya watoto wamefikiwa kupitia programu za kuboresha upatikanaji wa elimu, mafunzo kwa walimu, usambazaji wa vitabu na ujenzi wa miundombinu ya shule.
Kufikia mwaka 2024, GPE iliripoti kuwafikia watoto milioni 253, kutoa mafunzo kwa walimu milioni 1.9, kusambaza vitabu milioni 169 na kujenga au kukarabati zaidi ya madarasa 36,000.
Aidha, chini ya uenyekiti wa Dkt. Kikwete, GPE imepanua ushirikiano wake kwa kuongeza nchi wanachama na wadau wapya wa maendeleo.
Mwaka 2024, nchi za Jordan na Lebanon zilijiunga rasmi na ushirikiano huo, huku Saudi Arabia ikitangaza mchango mkubwa wa kifedha kwa ajili ya kuboresha elimu katika nchi zenye kipato cha chini.
Katika eneo la usawa wa kijinsia, GPE imeongeza juhudi za kuhakikisha wasichana wanapata fursa sawa za elimu ambapo pia shirika hilo limeimarisha programu za kuwajumuisha watoto wenye ulemavu, wakimbizi na makundi mengine yaliyokuwa yakibaki nyuma katika upatikanaji wa elimu.
Dkt. Kikwete ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania ameongoza juhudi za kuhamasisha ufadhili zaidi wa elimu duniani, akisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii
Kupitia mikutano yake mbalimbali ya kimataifa, Dkt Kikwete amekuwa mstari wa mbele kwenye kutetea uwekezaji mkubwa katika elimu ili kukabiliana na changamoto zilizotokana na athari za COVID-19, migogoro ya kimataifa na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa ujumla, kipindi cha uenyekiti wa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete GPE
imeonyesha mafanikio makubwa hasa katika kupanua fursa za elimu, kuimarisha ubora wa kujifunza, kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha watoto walio katika mazingira magumu wanapata haki yao ya msingi ya elimu bora.

No comments:
Post a Comment