Monday, June 29, 2026

POLISI MKOANI PWANI LINACHUNGUZA VIFO VYA MWANAMKE NA MTOTO

JESHI la Polisi Mkoani Pwani linafanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya mwanamke mmoja na mtoto ambao hawakufahamika yaliyotokea Mbwewe Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase kwa vyombo vya habari zilisema kuwa tukio hilo la mauaji ya watu wawili lililotokea Juni 2 mwaka huu  majira ya saa 9:00 alasiri huko Kitongoji cha Nung'uli Kijiji cha Kwang'andu Kata ya Mbwewe Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo.

Taarifa hiyo ilibainika kuwa watu hao ni mwanamke
mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka (20-25) na mtoto ambaye hakufahamika jinsia yake kutokana na kuungua sana na moto mwenye
umri unaokadiriwa kuwa miaka (3-6) ambao mpaka sasa bado hawajafahamika wala watu waliosababisha mauaji hayo.

"Ikumbukwe katika eneo la tukio hilo zilikutwa tiketi mbili za basi la Passion Video Coach linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam kwenda Miono kupitia Chalinze zilizokatwa tarehe Mei 31 mwaka huu,"alisema taarifa hiyo.

Taarifa zilisema kuwa tiketi hizo zilikiwa na majina ya Adela na Modest ambapo Jeshi bado linachunguza chanzo cha mauaji hayo wakati miili ya wahanga imehifadhiwa katika Hospitali ya Msoga Halmashauri ya Chalinze.

Kutokana na mauaji hayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea kutoa wito kwa mtu yeyote anayewafahamu watu hao au mwenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kuwatambua wafike Ofisi ya kamanda wa Polisi Mkoa
wa Pwani.

 "Au wapige simu namba 073900995, 065837601 0 na 0753855570 ili kuendelea kusaidia uchunguzi na kuwapata ndugu wa marehemu kwa wakati,"iliongeza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment