VIJANA wenye vipaji vya michezo nchini wametakiwa kusoma kwabidii na kuwa na nidhamu ili waweze kufikia viwango vya juu na kuwa tegemeo kwa Taifa.
Hayo yamesemwa na Gilbert Maregesi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha wakati wa kufunga tamasha la michezo lililoandaliwa na Compassion Kanda ya Mashariki lililofanyika kwenye Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Tumbi.
Maregesi amesema kuwa serikali imekuwa ikiwekeza kwenye sekta ya michezo kwa vijana ili kuendeleza vipaji vyao na kuwa tegemeo kwa Taifa kwenye sekta hiyo ambayo pia ni ajira kwa vijana.
"Ili kulinda vipaji vyenu mnapaswa kuwa na nidhamu ili muweze kufika mbali kwani mbali ya kunufaika binafsi pia mtaliwezesha Taifa kuwa na wachezaji wazuri watakaoliwakilisha Taifa kwenye michezo mbalimbali,"amesema Maregesi.
Naye mwakilishi wa meneja wa Compassion Kanda ya Mashariki Daudi Lawi inayoundwa na mikoa ya Pwani Morogoro na Dar es Salaam amesema tamasha hilo la awamu ya nne limeshirikisha wanamichezo 430 kutoka mikoa hiyo.
Lawi amesema kuwa baada ya kukamilisha tamasha hilo lilobeba ujumbe wa Kipaji changu Mtaji wangu watachaguliwa wachezaji bora ambao watawakilisha Kanda hiyo kwenye mashindano ya Taifa.
Kwa upande wake James Mhina Kanda ya Mlandizi ambao walikuwa wenyeji wa mashindano hayo amesema kuwa michezo hiyo inajenga mahusiano na kipaji ni msaada katika maisha.
Mwenyekiti wa Mashindano hayo Lucas Kiluwasha amesema kuwa vipaji vyao ndiyo mtaji wao hivyo wavitumie vizuri na kuwataka wadau wa michezo kushuhudia michezo ili wachukue vipaji na kuviendeleza.
Rais wa Vijana Kanda ya Mashariki amesema kuwa michezo hiyo imewasaidia kuwaongezea ujuzi na kukuza vipaji vyao na kujumuika na kufahamiana kwani hiyo ndiyo njia ya mafanikio.
Mgeni rasmi ametoa fursa ya vijana Milovan Kilingo kutoka Gairo na Joshua Joakim wa Mkuza Kibaha kujiunga na bendi ya Jkt Ruvu ili waendeleze vipaji vyao.
Baadhi ya michezo iliyochezwa ni pamoja na mpira wa miguu, pete, riadha na michezo ya ndani ikiwemo sanaa ya uimbaji, upigaji wa vyombo vya muziki, maonyesho ya mavazi na sarakasi na yalishirikisha vijana wenye umri chini ya mi 17 na 22.

No comments:
Post a Comment